Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato - Dodoma umefikia asilimia 54.1 kwa sehemu ya kwanza inayohusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, maegesho ya ndege, barabara za maungio na barabara za kuingia na kutoka kiwanjani ambapo unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Disemba, 2024.
Bashungwa ameeleza hayo leo, Machi 21, 2024 wakati akiwasilisha Utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa mwaka wa fedha 2023/24 na Makadirio ya Mpango na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
"Nikuhakikishie Mwenyekiti kuwa ujenzi wa uwanja huu sehemu ya kwanza unaendelea vizuri na mkandarasi anaendelea na kazi, sehemu ya pili inayohusisha ujenzi wa jengo la abiria na majengo mengine nayo imefikia asilimia 17.1", amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa amebainisha kuwa ukarabati, upanuzi na uboreshaji wa viwanja vya ndege vingine umefikia hatua mbalimbali ambapo Iringa (90%), Musoma (55%), Tabora (38%), Shinyanga (11%), Sumbawanga (6%) na Kiwanja cha Ndege cha Kigoma Mkandarasi yupo katika maandalizi ya kuanza ujenzi.
Bashungwa ameeleza kuwa Wakala wa Barabara (TANROADS) imefanikiwa kujenga barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa kilometa 134.75 za barabara kuu, kilometa 23.11 za barabara za Mikoa na ukarabati kwa kiwango cha changarawe kilometa 253.67 katika kipindi cha utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24.
Bashungwa ametaja baadhi ya miradi iliyotekelezwa ikiwemo ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi (km 3.2) na barabara unganishi (km 1.66) umefikia asilimia 85, ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Pili (km 20.3) umefikia asilimia 99.
Ameeleza miradi mingine ni ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje Dodoma (km 112.3) sehemu ya kwanza umefikia asilimia 68.3 na sehemu ya pili ya utekelezaji umefikia asilimia 56.32, upanuzi wa madaraja ya kibamba, kiluvya na mpiji yamekamilika pamoja na upanuzi wa barabara ya Kimara-Kibaha (km 19.2) njia nane.
Halikadhalika, Bashungwa amesema Wizara kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) imekamilisha ukarabati wa vivuko nane (8) ambavyo vinaendelea kutoa huduma maeneo mbalimbali, ukarabati wa vivuko vitatu (3) vipo katika hatua mbalimbali ya utekelezaji pamoja na ujenzi wa vivuko vipya sita vinaendelea.
Vilevile, Bashungwa amesema kuwa Wizara kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) imesajili Mkandarasi 1,192 ambapo Mkandarasi wa ndani ni 1,155 na wa nje ni 37 sawa na asilimia 99.3 ya lengo kwa mwaka 2023/24.
Hata hivyo, Bashingwa ameeleza Wizara kupitia Wakala wa Majengo (TBA) inaendeleza ujenzi wa majengo yenye uwezo wa kuchukua familia nyingi kutoka familia 4 hadi 114 katika maeneo yaliyokuwa chini ya usimamizi wa TAMISEMI ikiwemo Temeke Kota, Magomeni Kota na Ghana Kota.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mhe. Selemani Kakoso ameitaka Wizara kuendelea kusimamia na kutekekeleza miradi yote iliyoahidiwa na Serikali ili wananchi kupata huduma stahiki zinazotarajiwa.
Kadhalika, Kakoso ameisitiza Wizara hiyo kuendelea kufuatilia mchakato wa upatikanaji wa fedha ili kulipa madeni ya Makandarasi na kusaidia miradi mingine kuweza kutekelezwa kwa wingi na kwa wakati.
No comments:
Post a Comment