Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) ameiomba Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kuangalia uwezekano wa kuboresha Sheria yake ya Ununuzi ili miradi inayotekelezwa kupitia ufadhili wa Benki hiyo iweze kuwanufaisha wakandarasi wa ndani.
Dkt. Nchemba alitoa rai hiyo jijini Dodoma wakati wa mkutano kati yake na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya AfDB nchini Tanzania, Bi. Patricia Laverley, uliofanyika kwa njia ya mtandao ambao umeangazia namna bora ya kutekeleza na kukamilisha miradi ya maendeleo.
Alisema kuwa Tanzania imebadili Sheria zake za Ununuzi kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) mwaka 2023 ili kuwapa kipaumbele wakandarasi wa ndani kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi na kuzalisha walipakodi wakubwa ambao watakuwa sehemu ya ulipaji wa mikopo inayotolewa na Benki ya AfDB.
“Tulichojifunza katika tafiti tulizofanya ni kwamba kuna miradi mingi inayotekelezwa na kampuni za kigeni ikiwemo miradi ya miundombinu na huduma za kijamii ambapo wakandarasi wa ndani wananufaika kwa kiasi kidogo, uchambuzi unaonesha hali hiyo inakwamisha nchi yetu kutengeneza walipakodi wakubwa na kudhoofisha kukua kwa kampuni za ndani na hivyo kufifisha ukuaji wa sekta binafsi nchini”, alisema Dkt. Nchemba.
Alisema kuwa haileti picha nzuri inapoonekana deni linaendelea kukua kupitia utekelezaji wa miradi lakini wafadhili wanalipa fedha nyingi kwa kampuni za kigeni zinazotekeleza miradi ndani ya nchi wakati wakandarasi wadogo wanaoshiriki katika miradi kupitia kampuni zao hawanufaiki kikamilifu wakati wao ndio sehemu ya ulipaji wa deni kupitia kodi wanazotoa.
Dkt. Nchemba alisema kuwa inatakiwa kiasi kikubwa cha fedha kwenda kwa watanzania ili muda wa kulipa deni unapofika watambue kuwa kulikuwa na miradi imetekelezwa na walipata fedha kupitia kampuni zao.
Akizungumza kuhusu Miradi ya maendeleo, Dkt. Nchemba, alisema kuwa mkutano wake na Mwakilishi Mkazi wa Benki ya AfDB, umeangazia kwa kiasi kikubwa namna ya utekelezaji na ukamilishaji wa miradi ya maendeleo ukiwemo mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa Benki ya AfDB nchini Tanzania, Bi. Patricia Laverley, alisema kuwa Benki yake imepokea ombi la Tanzania la kuhakikisha wazawa wananufaika na fedha zinazotolewa na Benki hiyo kwenda kwenye miradi na itaangalia namna bora ya utekelezaji ikiwemo kuboresha Sheria zilizopo katika miradi ijayo ambayo haijasainiwa.
Alisema kuwa ni vema miradi ijayo ikaainisha namna sekta binafsi inavyoweza kushiriki katika utekelezaji wake na akaahidi Benki yake kuangalia uwezekano wa jambo hilo kutekelezwa kwa ufanisi.
No comments:
Post a Comment