EID JERUSALEM: HAKUNA SHEREHE, HAKUNA KUPAMBA NYUMBA ZETU-ILHAM. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, April 10, 2024

EID JERUSALEM: HAKUNA SHEREHE, HAKUNA KUPAMBA NYUMBA ZETU-ILHAM.

Ilham ni mmoja wa jumuiya ndogo ya Wapalestina ambao historia yao inafungamana na Msikiti wa al-Aqsa.

Waislamu wanasherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr ambayo inaadhimisha mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.


Lakini mwaka huu vita huko Gaza vimeleta huzuni kwenye sherehe hizo, haswa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel.


Wito wa adhana unasikika katika mitaa ya mji mkongwe wa Jerusalem Mashariki unaokaliwa kwa mabavu – wakati ukipita katika kituo cha ukaguzi cha Israel kabla ya kufika kwenye mlango wa nyumba ya Ilham mwenye umri wa miaka 35.


"Unasikia hiyo adhana?" anauliza kwa furaha. "Inatoka al-Aqsa."


Msikiti wa Al-Aqsa - mojawapo ya maeneo matakatifu zaidi katika Uislamu – upo karibu na nyumba yake.


Msikiti upo katika eneo linaloshindaniwa - likijuulikana kama Temple Mount, ambalo ni takatifu zaidi katika Uyahudi.


Ni fakhari kubwa kwake kuishi hapa.

"Ni zawadi ya kiroho," anasema. "Kila mtu ananionea wivu kwa hilo. Wananiambia, 'Una bahati sana!'


Mfanyakazi huyo wa kijamii ni mmoja wa Wapalestina wenye asili ya Afrika (Afro-Palestinians) wapatao 450, kutoka kizazi cha mahujaji kutoka Chad, Nigeria, Senegal na Sudan, wanaoishi katika eneo hili la Waislamu ndani ya mji mkongwe.


Nyumba zao ziliwahi kuwa magereza yaliyotumiwa na Dola la Otman kabla ya Uingereza kuchukua udhibiti wa Jerusalem mwaka 1917.


Miaka kadhaa baadaye, baada ya Uingereza kufanya jaribio lililoshindwa la kumuua Mufti Mkuu wa Jerusalem, Sheikh Haj Amin al-Husseini, alitoa ardhi hiyo kwa jumuiya ya Wapalestina wenye asili ya Afrika kama ishara ya nia njema.


Mlinzi kutoka jamii hiyo ndiye aliyeokoa maisha ya Mufti, na akapoteza maisha yake katika tukio hilo.

Jumuiya hiyo, ambayo imeishi katika eneo hilo kwa vizazi vitatu hadi vinne, sasa inajulikana kuwa walinzi wa al-Aqsa.


Mwaka huu, Ilham anasema, hakuna furaha yoyote inayoweza kuchukua nafasi ya unyonge wa Waislamu wa Palestina wanaoishi Jerusalem Mashariki.


"Unaweza kusema, 'Eid Njema,' na kukusanyika na kuketi na familia, lakini Eid gani?" Anauliza. "Hakuna Ramadhani, hakuna Eid. Kila kitu hakiko kama ilivyokuwa, katika maisha yetu ya kila siku. Tunakaa tu na kufikiria Gaza."



Wanawake hukusanyika kwenye Msikiti wa al-Aqsa kwa ajili ya swala ya Ijumaa.



Msikiti wa Al-Aqsa kila mara huwa na watu wengi kwa ajili ya swala ya Ijumaa, lakini Israel inazuia watu kufika wakati wa Ramadhani katika miaka ya hivi karibuni, kwa misingi ya usalama.


Mwaka huu, pamoja na mzozo wa Gaza, kulikuwa na hofu fulani kwamba mvutano ungezidi, na ilitangazwa kuwa wanaume wa zaidi ya umri wa miaka 55 na wanawake wa zaidi ya umri wa miaka 50 ndio wataruhusiwa kuingia.


Licha ya hayo, walinzi waliowekwa nje wameruhusu maelfu ya wageni wa rika zote kukusanyika kuswali katika eneo ambalo wanaamini Mtume Muhammad alipaa kwenda mbinguni.


Ilham mwenyewe anaingia bila shida. Huingia katikati ya uwanja wa msikiti huo, na kuketi akiwa miongoni mwa maelfu ya wanawake walioketi kwa ajili ya swala.


Imam anaanza na khutba. Jambo moja tu liko akilini mwake. "Baridi kali, viungo vya binaadamu na chemchemi za damu kutoka ardhi yetu pendwa, Gaza. Tunatafuta kimbilio kwa Mungu kutoka kwa mioyo migumu kama mawe, isiyo na huruma, rehema, na ubinadamu. Mungu isaidie Gaza."


Kila mtu anaiombea Gaza. Maombi ni aina nyingine ya upinzani. 


Prof Mustafa Abu Sway, ambaye anafundisha katika msikiti huo, anasema Waislamu wa Jerusalem Mashariki wamevunjika moyo.


"Ramadhan ni mwezi wa kiroho, kujitathmini, kutoa na kuwatunza dada na kaka zetu katika ubinadamu, wakati tunaendelea kufanya kadiri tuwezavyo, Ramadhani hii imefunikwa na mauaji ya halaiki huko Gaza ambapo kila kitu kinakosekana isipokuwa vifo, njaa na maumivu."


Israel inasema tuhuma za mauaji ya halaiki ni ya kuudhi na kwamba inafuata sheria za kimataifa bila kuyumba.



Ilham na familia yake wakipata futari baada ya jua kuzama huko Jerusalem Mashariki.



Katika matembezi yake ya dakika moja kurudi nyumbani, Ilham anapita kwenye maduka ya soko katika vichochoro vya eneo hili la Waislamu.


Anapoingia katika mtaa wake, kuta za zimechorwa. 


Mchoro mmoja unaonyesha bara la Afrika, pia kukiwa na mchoro wa ramani ya Palestina iliyoambatanishwa na Misri.


Amefika nyumbani kwake muda muafaka kwa ajili ya futari - pamoja na familia yake, ikiwa ni pamoja na wajomba zake na shangazi zake. Nyumba ina shughuli nyingi na mazungumzo yametawaliwa na mama yake na shangazi zake.


Walipokuwa wakijiandaa kula mazungumzo yanabadilika kutoka mambo ya kijamii na siku yao ilivyokwenda kwenye ibada zao.


Kisha mazungumzo yanabadilika na kuwa vita vya Gaza. Shangazi yake Ilham anasema: "Ee Mungu, tunakula, chini ya paa la nyumba. Ee Mungu hapa hakuna baridi."


Eid hii, wanachama wa jumuiya ya Afro-Palestina wanasema wanaonyesha mshikamano na wale wa Gaza. Ndiyo maana Eid itaadhimishwa kwa jina tu.


"Hakuna sherehe," Ilham anasema. "Hatujapamba nyumba zetu, hakuna wageni. Ni mambo ya kiroho na kiibada tu kuhusu Ramadhani ndio yamebaki."

No comments:

Post a Comment