Jeshi la Israel limesema liko tayari kukabiliana na tishio lolote la Iran, huku hali ya wasiwasi ikiongezeka baada ya shambulio la Jumatatu kwenye ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus.
Israel inaaminika kuhusika na shambulio hilo, ambalo Iran ilisema liliua maafisa saba wa kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi.
Afisa wa Iran alisema siku ya Jumapili kuwa balozi za Israel "haziko salama tena", huku ikitayarisha majibu.
Vikosi vya Marekani na Israel katika eneo hilo vimewekwa katika hali ya tahadhari kwa kutarajia mashambulizi yanayoweza kutokea.
Ripoti katika vyombo vya habari vya Marekani zinaonyesha kwamba hatua ya kulipiza kisasi kutoka Iran inaweza kutokea katika siku zijazo.
"IDF [Vikosi vya Ulinzi vya Israel] vinaweza kushughulikia Iran," Mkuu wa Majeshi ya Israel Herzi Halevi alisema katika taarifa yake kwa njia ya televisheni. "Tunaweza kuchukua hatua kwa nguvu dhidi ya Iran katika maeneo ya karibu na mbali."
Yahya Rahim Safavi, mshauri mkuu wa Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei, alisema Iran ina "haki ya kisheria na halali" ya kujibu shambulio la Jumatatu.
"Balozi za utawala wa Kizayuni haziko salama tena," aliliambia shirika la habari la Isna la Iran. Hakutoa maelezo zaidi kuhusu majibu ya Iran yatakuwa ya aina gani.
Katika taarifa yake, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant alisema idara ya ulinzi imekamilisha maandalizi ya kukabiliana na hali yoyote inayoweza kutokea.
IDF imesitisha likizo zote kwa wanajeshi wanaohudumu katika vitengo vya mapigano na kuwaita askari wa akiba ili kuimarisha ulinzi wa anga.
Israel pia imezuia mawimbi ya GPS katika maeneo yote ya nchi ili kutatiza makombora na ndege zisizo na rubani.
Vyombo vya habari nchini Israel vimeripoti kuwa baadhi ya balozi za nchi hiyo zilihamishwa kutokana na tishio la mashambulizi ya Iran.
BBC haijathibitisha taarifa hizo kwa njia uhuru na Israel haijazithibitisha, pia katika juhudi zinazoonekana za kuzuia hofu, msemaji wa jeshi la Israel alisema hakuna haja ya watu kununua jenereta, kukusanya chakula au kutoa pesa.
Wizara ya ulinzi ya Syria ilisema ndege za Israel zililenga jengo la ubalozi mdogo wa Iran saa 17:00 saa za huko (14:00 GMT) siku ya Jumatatu.
Vikosi vya ulinzi vya anga vya Syria vilidungua baadhi ya makombora, lakini mengine yalifanikiwa na "kuharibu jengo zima, na kuua na kujeruhi kila watu ndani", wizara hiyo iliongeza.
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran limesema kuwa maafisa wake saba waliuawa katika shambulio hilo akiwemo Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi na Brigedia Jenerali Mohammad Hadi Haji-Rahimi.
Picha na video kutoka eneo la tukio zilionyesha moshi ukipaa kutoka kwenye mabaki ya jengo lililoporomoka. Saa chache baada ya shambulio hilo, watu mjini Tehran walichoma moto bendera za Israel na Marekani katika maandamano.
Siku moja baada ya shambulio hilo, Ayatollah Khamenei alisema Israel "itajutia uhalifu huu", huku Rais Ebrahim Raisi akisisitiza "haitakosa jibu".
Israel na mshirika wake wa karibu, Marekani, wamekuwa wakitarajia mashambulizi ya Iran tangu wakati huo.
Kutokana na shambulio hilo, jeshi la Israel lilisema halikuzungumzia taarifa za vyombo vya habari vya kigeni.
Lakini afisa mmoja mkuu wa Israel ambaye jina lake halikutajwa ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba waliouawa "wamekuwa nyuma ya mashambulizi mengi dhidi ya mali ya Israel na Marekani na walikuwa na mipango ya mashambulizi ya zaidi". Pia walisisitiza kuwa ubalozi huo "haukuwa lengo".
Israel imekiri kutekeleza mamia ya mashambulizi katika miaka ya hivi karibuni kwenye shabaha nchini Syria ambayo inasema inahusishwa na Iran na makundi washirika ambayo yana silaha, yanayofadhiliwa na kupewa mafunzo na jeshi la iran la Walinzi wa Mapinduzi.
Iran imesema walinzi hao walitumwa Syria "kushauri" vikosi vya Rais Bashar al-Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo, lakini imekanusha kuwa wamehusika katika mapigano au kuanzisha vituo.
Mashambulizi ya Israel yameripotiwa kuongezeka tangu kuanza kwa vita huko Gaza mwezi Oktoba mwaka jana, kujibu mashambulizi ya kuvuka mpaka kaskazini mwa Israel yaliyofanywa na Hezbollah na makundi mengine yanayoungwa mkono na Iran huko Lebanon na Syria.
Iran imeepuka makabiliano ya moja kwa moja na Israel wakati wa mzozo hadi sasa, lakini shambulio la Jumatatu linaonekana kama ongezeko kubwa.
No comments:
Post a Comment