Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. MUSSA Ally Mussa kulia akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo katika kikao kilichofanyika ofisini kwake tarehe 22 Aprili, 2024 |
Na Mwandishi Wetu Morogoro
Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ally Mussa ameahidi kuwa mkoa wake utashiriki kikamilifu katika kuhamasisha matumizi ya mbolea na kusaidia kuondoa imani potofu kuwa udongo wanaoulima una rutuba ya kutosha na kusababisha matumizi hafifu ya mbolea.
Amesema wakulima wengi wanaamini udongo wao unarutuba kutokana na kupokea rutuba inayosafirishwa kutoka milimani wakati wa mvua kubwa.
Dkt. Mussa amesema hayo tarehe 22 Aprili, 2024 alipokuwa akizungumza na Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ilipofanya ziara ofisini kwake iliyolenga kuhamasisha Ofisi za Mkoa kushiriki katika kuhamasisha matumizi ya mbolea pamoja na kupima afya ya udongo ya watu wake kupitia vifaa vilivyogawiwa na Wizara kwa Maafisa Ugani wa Kata zote nchini.
changamoto nyingine ni uelewa mdogo wa matumizi sahihi ya mbolea na jiografia ya mkoa ni suala jingine linalosababisha matumizi hayo kuwa hafifu.
Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Bodi ya TFRA, Dkt. Anthony Diallo aliiomba Ofisi ya Mkoa kuhimiza maafisa ugani ndani ya mkoa huo kupima afya ya udongo na kuwasilisha taarifa za upimaji huo ili kuwasaidia wakulima kujua aina ya mbolea wanayopaswa kutumia kulingana na mahitaji ya udongo na hivyo kuongeza tija.
Aidha, ameomba uongozi wa mkoa huo kuwashirikisha wafanyabiashara wa mbolea kwenye vikao vya pembejeo ili wapate maoni yao kabla ya kuwasilisha TFRA ili yazingatiwe wakati wa kupanga bei elekezi na hivyo zilingane na umbali wa maeneo wanakofikisha bidhaa hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent ameuomba uongozi wa Mkoa kuhimiza wananchi wake kujisajili ili waweze kunufaika na ruzuku ya mbolea inayotolewa na serikali ili kuwapa ahueni ya gharama za uzalishaji wakulima.
Amesema mpaka kufikia tarehe 14 Aprili, 2024 jumla ya wakulima 138,538 wamesajiliwa kwenye mfumo wa mbolea za ruzuku na wanufaika wa mpango huo ni wakulima 13,653 walionunua kiasi cha tani10,808.15 za mbolea.
Akiwasilisha ombi la wafanyabiashara wa mbolea katika kikao baina yao na TFRA Mwenyekiti wa Chama cha wafanyabiashara wa Mbolea, Gerold Mlenge aliiomba Mamlaka kupanga bei elekezi kulingana na umbali halisi wa maeneo inakopaswa kufika kwani maeneo mengi ya mkoa huo yako mbali na makao makuu ya wilaya ili waone faida ya kufanya biashara hiyo na wakulima wafikishiwe bidhaa hiyo karibu na maeneo yao.
No comments:
Post a Comment