Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kilimo, Obadia Nyagiro,akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa Kilimo Ikolojia hai kilichoratibiwa chini ya mwamvuli wa Taasisi za Kilimo Hai Tanzania (TOAM) kilichofanyika jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa TOAM, Dk.Mwatima Juma,akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa Kilimo Ikolojia hai kilichoratibiwa chini ya mwamvuli wa Taasisi za Kilimo Hai Tanzania (TOAM) kilichofanyika jijini Dodoma.
Paul Holmbeck kutoka Shirika la Biovision Foundation,akizungumza wakati wa kikao cha wadau wa Kilimo Ikolojia hai kilichoratibiwa chini ya mwamvuli wa Taasisi za Kilimo Hai Tanzania (TOAM) kilichofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ywa wadau wa Kilimo Ikolojia hai wakifatilia majadiliano mbalimbali wakati wa kikao hicho kilichoratibiwa chini ya mwamvuli wa Taasisi za Kilimo Hai Tanzania (TOAM) kilichofanyika jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WADAU wa kilimo ikolojia hai wamekutana jijini Dodoma kutengeneza mpango kazi wa mwaka 2024/25 kwa ajili ya utekelezaji vipaumbele vya Mkakati wa kitaifa wa kilimo hai wa ikolojia wa 2023-2030 (NEOAS) utakaoleta mageuzi ya kilimo nchini.
Akizungumza kwenye kikao hicho kilichoratibiwa chini ya mwamvuli wa Taasisi za Kilimo Hai Tanzania (TOAM), Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara ya Kilimo, Obadia Nyagiro, alisema kilimo hicho ni muhimu kwa watanzania kwa kuwa kitaleta tija kiuchumi, kulinda afya za walaji, afya ya udongo na kuongeza kipato.
Alisema mkakati huo unatokana na Sera ya kilimo kuelekeza masuala ya kuweka mfumo wa uzalishaji, upatikanaji wa masoko na kutambua bidhaa za kilimo hai.
“Mkakati wenyewe ulizinduliwa mwishoni mwa mwaka jana na upo tayari kwa utekelezaji, kilichotufanya tukutane ni namna ya kutekeleza mkakati huu kwa kuandaa mpango kazi kila mwaka kwa muda wa miaka saba ya huu mkakati wa kitaifa, kama tulivyowashirikisha kwenye maandalizi yake lazima tushiriki sisi wadau kwa kuweka malengo ya utekelezaji wake kila mwaka,”alisema.
Alisema serikali itaendelea kutoa ushirikiano ili kufanikisha uandaaji wa mpango huo kwa kuwa ni muhimu wadau kushiriki katika kilimo himilivu na endelevu kwa mazingira na afya ili kuleta tija kwenye sekta ya kilimo.
Alizitaka asasi za kiraia na sekta binafsi kuchangamkia fursa ya uwekezaji katika kilimo hicho kwa kuwa kina tija kubwa.
“Nihimize sekta binafsi na asasi za kiraia mpitie na kuona fursa ya kuwekeza katika eneo hili kwa kuwa tija yake ni kubwa ikiwamo kuongezeka kwa mapato, mkipitia nchi nyingine mtaona waliowekeza kwenye kilimo hiki na tija yake na ni muhimu mipango yetu izingatie kilimo himilivu kinachozingatia mabadiliko ya tabia nchini,”alisema.
Naye, Mwenyekiti wa TOAM, Dk.Mwatima Juma alisema kilimo hicho kinalenga kuwa na uzalishaji wa kutosheleza, kulinda afya na udongo kwa kuondokana na matumizi ya kemikali.
“Kilimo cha kutumia kemikali kilianza miaka 100 iliyopita baada ya kuisha kwa vita kuu ya pili ya dunia ambapo utengenezaji wa mbolea za kemikali, viuatilifu vya kemikali ilionekana itatusaidia kuzalisha chakula zaidi, tulihamasika kuwa kutumika kemikali ndo ukisasa na kwa bahati mbaya tuliacha kilimo chetu cha asili ambacho mtu alikuwa akilima kahawa ndani yake ana kunde,maharage, mtama vyote vinazalishika vizuri na ana ng’ombe anatupia mbolea shambani kwake.”
“Tukahamasisha tuwe na mashamba makubwa tulime zao moja, tupulize dawa miaka imekwenda na tulipofika mimi binafsi nasema tuwaombe radhi wakulima kwa maeneo tuliyowapeleka hasa wakulima wadogo hapafai, kuna aina ya ukulima wanaweza kulima bila kupunguza uzalishaji, bila kupata shida kwenye chakula na kuuza kwenye masoko ya ndani na nje,”alisema.
Alibainisha kuwa kilimo hicho kitasaidia watanzania kuondokana na maradhi mbalimbali ikiwamo uzazi, saratani kwa kuwa yanatokana na matumizi ya kemikali kwenye kilimo.
Naye, Paul Holmbeck kutoka Shirika la Biovision Foundation akizungumzia mataifa mengine namna yanavyotekeleza kilimo hicho, alisema wanasayansi na mashirika ya kimataifa ya masuala ya kilimo yanahimiza kilimo hicho kwa usalama wa chakula na kuna tija kiuchumi ambapo serikali za nchi ambazo zinatekeleza kilimo hicho zinaweka malengo yake.
No comments:
Post a Comment