WANAFUNZI WAPEWE ELIMU YA MATUKIO YA DHARURA: WAZIRI BASHUNGWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, April 19, 2024

WANAFUNZI WAPEWE ELIMU YA MATUKIO YA DHARURA: WAZIRI BASHUNGWA


Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Viongozi na Wasimamizi wa Shule za Serikali na binafsi kutoa elimu kuhusu matukio ya dharura yanayoweza kutokea katika mazingira ya shule ikiwa ni pamoja na elimu juu ya majanga ya moto ambayo yamekuwa yakitokea.

Bashungwa ameeleza hayo leo tarehe 19 Aprili 2024 mara baada ya kuzindua Bweni jipya la Wavulana katika Shule ya Msingi ya Kingereza KARADEA katika Kata ya Bugene Wilaya Karagwe.


“Ujenzi wa Bweni umezingatia masuala ya dharura pia niwaombe hata kama dharura haipo tutengeneze mazingira ya dharura ambayo yatawawezesha kupata elimu kuhusu matukio hayo”, amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa amelipongeza Shirika la KARADEA kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika shule hiyo na ameahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi ambazo zimeendelea kuwa na mchango mkubwa kwa jamii ya Watanzania.

Bashungwa amechangia mabati 100 ambayo yatawezesha ujenzi wa madarasa katika shule hiyo ili kuboresha mazingira ya wanafunzi kujifunza na kufundishwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule Lenadius Lemingthon amesema Bweni lililozinduliwa lina uwezo wa kulaza wanafunzi 320 na lina mahitaji yote muhimu kwa wanafunzi ikiwemo vyoo, bafu, maeneo ya kufulia pamoja na vifaa vinavyotumika wakati wa dharura.

No comments:

Post a Comment