BASHUNGWA AWAPONGEZA MAMENEJA TANROADS, UREJESHWA WA MAWASILIANO YA BARABARA ILIYOHARIBIWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 31, 2024

BASHUNGWA AWAPONGEZA MAMENEJA TANROADS, UREJESHWA WA MAWASILIANO YA BARABARA ILIYOHARIBIWA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewapongeza Mameneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) mikoa yote nchini kwa jitihada kubwa walizozifanya za kurejesha mawasiliano ya miundombinu ya barabara na madaraja yaliyokatika katika kipindi cha Mvua za El Nino zilizoambatana na Kimbunga Hidaya kwa haraka.

Bashungwa ametoa pongezi hizo Mei 31, 2024 jijini Dodoma katika kikao cha majumuisho kilichokutanisha Menejimenti ya Wizara, Wakuu na Menejimenti za Taasisi zilizo chini ya Wizara pamoja na Mameneja wa Wakala ya Barabara (TANROADS) nchi nzima, Mameneja wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) na Mameneja wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambapo amesisitiza urejesha wa miundombinu hiyo uliwezesha wananchi kuendelea na shughuli za usafiri na usafirishaji kama ilivyokuwa awali.

“Niipongeze Wizara, timu nzima ya TANROADS bila kumsahau Mkurugenzi wa Matengenezo kwa jitihada mlizochukua wakati wa kipindi cha mvua za mafuriko na Kimbunga Hidaya katika mikoa yote nchini hakika mmeupiga mwingi,” amesema Bashungwa.

Bashungwa ameagiza Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) kukamilisha mwongozo wa Sekta ya Ujenzi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo kukabiliana na mafuriko na majanga ya asili katika miundombinu ya barabara na madaraja ili kusaidia Serikali kutekeleza na kubuni mipango yake kwa ufanisi katika miundombinu hiyo.

Bashungwa amewataka TBA kuangalia namna bora ya kujenga nyumba za bei nafuu zitakazoweza kusaidia Watumishi wa Umma katika Halmashauri kupata nyumba bora na nafuu karibu na maeneo yao ya kazi.

Bashungwa ameagiza TEMESA kuanza kujipanga katika mwaka mpya wa fedha 2024/25 unaotarajia kuanza mwezi Julai, 2024 kujiendesha kibiashara na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Aidha, Bashungwa ameziagiza kila Taasisi kuchukua mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bunge ya Miundombinu katika uwasilishwaji wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2024/25 na kuyaweka katika mipango yao ya kazi kwa ajili ya utekelezaji.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa ujenzi Mheshimiwa Godfrey Kasekenya amewaasa watumishi wa Wizara hiyo kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu na kuzingatia viwango vya ubora katika utekelezaji wa miradi nchini ili kujenga uhusiano imara kwa wadau ambao wanapata huduma kutoka kwa Wizara na Taasisi zake.

"Hakikisheni mnaendelea kufanya kazi kwa bidii na uzalendo, msiridhike kwa sifa mnazozipata, sifa hizi ziwajenge ili kuchapa kazi zaidi ili kufikia malengo ya kuendeleza na kukuza sekta ya Ujenzi," amesema Mheshimiwa Kasekenya.

Ameelekeza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kujipanga na kujiimarisha katika utekelezaji wa majukumu yao na kutafuta ufumbuzi wa haraka pindi changamoto zinapojitokeza wasisubiri hadi kupata lawama kwa wananchi.

No comments:

Post a Comment