Na Carlos Claudio,Dodoma.
Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amefungua kongamano la kwanza la kisayansi la afya la Chuo Kikuu cha Dodoma UDOM huku akihimiza jamii kutenga siku maalum ya kufanya mazoezi ili kuweza kupambana na tatizo la uzito uliozidi.
Dkt. Mollel ameyasema hayo Mei 29, 2024 jijini Dodoma akieleza kwa kufanya mazoezi angalau mara tatu kwa wiki kwa muda usiyopungua dakika 30 utaweza kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa kama kisukari, shinikizo la damu pamoja na uzito uliozidi.
Lengo la mkutano huo ni kujadili maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG3) iliyopitishwa mwaka 2015 inayolenga kuhakikisha maisha yenye afya na ustawi kwa wote kufikia 2030.
“Ili kufikia lengo hili kubwa lakini muhimu, Umoja wa Mataifa (UN) ulihimiza nchi kuchukua hatua za ujasiri na ahadi za kushughulikia sababu kuu za afya mbaya na vifo vya mapema, ahadi hizi ni pamoja na kupunguza vifo vya uzazi duniani hadi kufikia chini ya 70/100,000, na kupunguza vifo vya watoto wachanga na watoto chini ya umri wa miaka mitano hadi kufikia chini ya 12/1000 na 25/1000 wanaojifungua,”
“Kushughulikia changamoto za afya ya umma kama vile vifo vya uzazi na watoto; magonjwa ya kuambukiza kama vile VVU/UKIMWI, kifua kikuu na Malaria, magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama vile kisukari, magonjwa ya moyo na mishipa, afya ya akili na ajali za barabarani, upatikanaji na upatikanaji wa huduma bora za afya; na ufadhili wa huduma za afya ni muhimu kwa mafanikio ya maisha yenye afya na ustawi kwa wote.” amesema Mollel.
Mollel amesema kuwa athari kubwa zaidi katika nchi za kipato cha kati na cha chini zimesababisha magonjwa yasiyo ya kuambukizwa kama vile magonjwa ya moyo, saratani, kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya mapafu na magonjwa ya figo yanaongoza kwa kusababisha vifo na ulemavu duniani kote.
Kwa upande wa makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma profesa Lughano Kusiluka amesema Dodoma inahitaji vituo vikubwa vya magonjwa na upandikizaji wa figo kama ilivyo awali kwani tangu huduma ya upandikizaji figo ianze mkoani Dodoma imeweza kupandikiza figo wagonjwa 40 na kupunguza gharama za wagojwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Profesa Kusiluka amehimiza wanataaluma, watafiti na wadau wa afya kuweka lengo la kuijenga Tanzania yenye afya ili kujenga kizazi timamu ambacho kitapelekea kukuza uchumi wa nchi.
“Kila mwaka huwa tunatembelea Nyerere Square kuwapata watu wa Dodoma, kwaio sisi kila mwaka wakati wa kuadhimisha siku ya figo duniani huwa tunatoa huduma pale, mwaka jana tulikwepo pale tukahudumia watu kama 800 na mwaka huu tumeweza kuhudumia watu 800,”
Kusiluka ameongeza kuwa, “ Tumekuwa tukishirikiana sana na wadau wetu hapa Dodoma, hospitali zote lakini tumekuwa tukishirikiana sana na wenzetu wa hospitali ya Benjamin Mkapa kwasababu ilijengwa kwaajili ya kusaidia ufundishaji na hilo tunalitambua vizuri na tunafahamu huduma za upandikizaji figo imefanywa kwa ukaribu sana kati ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma na hopitali ya Benjamin Mkapa.
Aidha amehimiza wanataaluma, watafiti na wadau wa afya kuwa na tabia ya kubadilishana ujuzi na uzoefu katika masuala ya afya pamoja na kutafakari mchango wao kwenye maisha yenye ustawi bora kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment