DKT NCHEMBA AUSHUKURU UMOJA WA ULAYA KWA KUSAIDIA MAENDELEO YA NCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 24, 2024

DKT NCHEMBA AUSHUKURU UMOJA WA ULAYA KWA KUSAIDIA MAENDELEO YA NCHI

Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa mgeni rasmi wakati wa maadhimisho ya Siku ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya ambapo ameushukuru Umoja huo kwa mchango wake katika maendeleo ya nchi kupitia misaada na mikopo yenye masharti nafuu ambapo hadi sasa uwekezaji wa Umoja huo umefikia thamani ya euro bilioni 3 sawa na takriban shilingi trilioni 8 za Tanzania. Maadhimisho hayo yamefanyika katika Makazi ya Balozi wa Umoja huo, Mhe. Christine Grau, Jijini Dar es Salaam.


Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam


Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameishukuru Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kwa mchango wake katika maendeleo ya Tanzania, kupitia misaada na mikopo yenye masharti nafuu ambapo hadi sasa uwekezaji wa Umoja huo umefikia thamani ya euro bilioni 3 sawa na takriban shilingi trilioni 8 za Tanzania.

Dkt. Nchemba (Mb), amesema hayo wakati akiongoza maadhimisho ya Siku ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya yaliyofanyika katika Makazi ya Balozi wa Umoja huo, Mhe. Christine Grau, Jijini Dar es Salaam.

Alifafanua kuwa euro bilioni 2.4 sawa na shilingi trilioni 6.4 ni msaada na kiasi kingine cha euro milioni 573 sawa na shilingi trilioni 1.5 ni mkopo wenye masharti nafuu uliotolewa na Benki ya Uwekezaji ya Jumuiya ya Umoja wa Ulaya (European Investment Bank-EIB) ambazo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta za usafiri, nishati, kilimo, biashara na uwekezaji, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, maji na usafi wa mazingira.

Aidha, Dkt. Nchemba aliishukuru Jumuiya hiyo kwa kutenga kiasi cha euro bilioni 300 kupitia mpango wake wa Global Gateway, kwa ajili ya mikakati ya kukuza uwekezaji ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 150 zimetengewa nchi za kiafrika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu pamoja na mifumo ya kidigiti.

“Msaada huo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo na utengamano wa nchi zetu, kukuza uchumi, na maendeleo ya wananchi kwa ujumla” alisema Dkt. Nchemba


Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania, ikiongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaendelea kufanya maboresho ya sera na mikakati mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya nchi pamoja na kutekeleza miradi ya kimkakati, ikiwemo utalii wa kimataifa na kilimo kupitia program ya Build a Better Tomorrow (BBT), unaolenga kuongeza uzalishaji na kukuza ajira kwa vijana.

Kwa upande wake, Balozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Mhe. Christine Grau, aliipongeza Tanzania kwa hatua mbalimbali inazochukua kukuza uchumi na maendeleo ya nchi na watu wake na kuahidi kuwa umoja huo utaendelea kushiriki katika kukuza zaidi maendeleo hayo kupitia uwekezaji wa mitaji kupitia misaada na mikopo nafuu pamoja na kuhamasisha uwekezaji kupitia kampuni zilizoko kwenye nchi wanachama za umoja huo.

Aidha, Mhe. Grau alifafanua kuwa uwekezaji wa euro bilioni 300 kupitia mpango wa Global Gateway ambao utainufaisha pia Tanzania, umelenga kukuza uchumi wa kidijiti, kuongeza uwekezaji na kukuza sekta muhimu za ujenzi wa miundombinu itakayochochea uzalishaji na kuongeza mnyororo wa thamani ili kuyafikia masoko ya kimataifa, ujenzi wa miji salama na ya kijani.

No comments:

Post a Comment