Korea Kusini hivi majuzi ilidai kuwa Korea Kaskazini ilituma makontena 6,700 ya silaha nchini Urusi.
Januari 2, mkaguzi wa silaha wa Ukraine, Khrystyna Kimachuk, alipata habari kwamba kombora lenye sura isiyo ya kawaida lilikuwa limeanguka kwenye jengo katika jiji la Kharkiv.
Alianza kuwasiliana na jeshi la Ukraine, akitamani sana kulijadili. Ndani ya wiki moja, alikuwa na vipande vya kombora mbele yake mahali fulani katika mji mkuu, Kyiv.
Kimachuk alianza kupiga picha kila kipande, ikiwa ni pamoja na chipu za kompyuta ambazo zilikuwa ndogo kuliko kucha zake. Mara moja aligundua halikuwa kombora la Urusi, lakini ilibidi athibitishe.
Kimachuk aliona herufi ndogo kutoka alfabeti za Kikorea. Kisha akapata maelezo ya wazi zaidi.
Nambari 112 ilikuwa imechapwa kwenye sehemu ya kombora. Hii inalingana na mwaka 2023 katika kalenda ya Korea Kaskazini.
Hivyo, alitambua kwamba kuna ushahidi wa kwanza kabisa kwamba silaha za Korea Kaskazini zilitumiwa kushambulia nchi yake.
Tangu wakati huo, jeshi la Ukraine linasema Urusi imerusha makumi ya makombora ya Korea Kaskazini katika eneo lake. Yameuwa takribani watu 24 na kujeruhi zaidi ya 70.
Kimachuk anafanya kazi katika Shirika la Utafiti wa Silaha (CAR), ambalo linachukua silaha zinazotumiwa vitani, ili kugundua jinsi zilivyotengenezwa.
Kombora lilijaa vifaa vya teknolojia ya kisasa. Sehemu nyingi za kielektroniki zinatoka Marekani na Ulaya. Kulikuwa na hata chipu ya kompyuta ya Marekani iliyoundwa Machi 2023.
Hii ilimaanisha Korea Kaskazini ilinunua kwa njia haramu vifaa muhimu vya silaha, ikaviingiza nchini humo, ikatengeneza kombora hilo, na kulisafirisha kwa siri hadi Urusi.
"Hili lilikuwa jambo la kushangaza zaidi. Licha ya kuwa chini ya vikwazo vikali kwa karibu miongo miwili, Korea Kaskazini bado inaweza kupata kila inachohitaji kutengeneza silaha zake, na kwa kasi ya ajabu," anasema Damien Spleeters, naibu mkurugenzi wa CAR.
Huko London, Joseph Byrne, mtaalamu wa Korea Kaskazini katika Taasisi ya Royal United Services Institute (RUSI), ambaye amekuwa akifuatilia hali ya mambo.
Kwa kutumia picha za satelaiti, wameweza kutazama meli nne za mizigo za Urusi zikienda na kurudi kati ya Korea Kaskazini na bandari ya kijeshi ya Urusi, zikiwa zimesheheni mamia ya makontena.
Kwa jumla, RUSI inakadiria makontena 7,000 yamesafirishwa, yakiwa na risasi zaidi ya milioni na roketi za Grad, ambazo zinaweza kurushwa kutoka katika lori.
Tathmini yao inaungwa mkono na ujasusi kutoka Marekani, Uingereza na Korea Kusini, ingawa Urusi na Korea Kaskazini zimekanusha biashara hiyo.
Tangu miaka ya 1980, Korea Kaskazini imeuza silaha zake nje ya nchi, hasa kwa nchi za Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati, ikiwa ni pamoja na Libya, Syria na Iran. Kawaida ni makombora ya zamani, ya mtindo wa Soviet yasiyofanya kazi vizuri.
Kuna Imani kuwa wapiganaji wa Hamas huenda walitumia baadhi ya makombora ya zamani ya Pyongyang katika shambulio lao la Oktoba 7.
Lakini kombora lililorushwa Januari 2 ambalo Kimachuk lilikuwa ni kombora la kisasa zaidi la masafa mafupi la Pyongyang, Hwasong 11, lenye uwezo wa kusafiri hadi kilomita 700.
Dk. Jeffrey Lewis, mtaalamu wa silaha za Korea Kaskazini katika Taasisi ya Mafunzo ya Kimataifa ya Middlebury, anasema, ‘faida ya makombora haya ni kwamba ni nafuu sana. Hii ina maana unaweza kununua kwa wingi na kuyatumia kwa wingi ili kuharibu ulinzi wa anga, jambo ambalo Urusi inaonekana kulifanya.”
Anaamini viwanda vya kutengeneza silaha vya Pyongyang vikifanya kazi kwa uwezo kamili, vinaweza kuzalisha takribani makombora mia moja kwa mwaka.
Nyingi za chipu za kompyuta ambazo ni muhimu kwa silaha za kisasa, zinazopaa na kupiga shabaha, ni sawa na chipu zinazotumiwa katika simu zetu, mashine za kuosha nguo na magari.
Hizi zinauzwa kote ulimwenguni kwa idadi kubwa. Watengenezaji huzitengeneza na kuzisambaza, ikimaanisha mara nyingi hawajui bidhaa zao zinaishia wapi.
Wakorea Kaskazini walio ng'ambo walianzisha kampuni ghushi huko Hong Kong na nchi nyingine za Asia ya Kati ili kununua bidhaa hasa kwa kutumia pesa zilizoibwa.
Kisha husafirisha bidhaa hadi Korea Kaskazini, kwa kawaida katika mpaka wake na China. Ikiwa kampuni bandia itagunduliwa na kuwekewa vikwazo, kampuni nyingine huziba nafasi yake haraka.
Vikwazo kwa muda mrefu vimezingatiwa kuwa njia ya kupambana na mitandao hii, lakini ili kufanikiwa ni lazima vikwazo vitekelezwe mara kwa mara.
Lakini Urusi na China zimekataa kuiwekea Korea Kaskazini vikwazo vipya tangu 2017.
Kwa kununua silaha kutoka Pyongyang, Moscow inakiuka vikwazo ilivyowahi kuvipigia kura kama mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Fauka ya hilo, mapema mwaka huu, Urusi ilifuta kikamilifu jopo la Umoja wa Mataifa la ufuatiliaji ukiukaji wa vikwazo, ili kuepuka kuchunguzwa.
"Tumeshuhudia kufutwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Korea Kaskazini, na kuipa Pyongyang nafasi kubwa ya kupumua," anasema Byrne.
"Washindi wa kweli hapa ni Korea Kaskazini," Byrne anasema. "Imeisaidi Urusi kwa kiasi kikubwa, na hii imewapa ushawishi mkubwa."
Mwezi Machi, RUSI iliandika juu ya kiasi kikubwa cha mafuta yaliyokuwa yakisafirishwa kutoka Urusi hadi Korea Kaskazini, huku mabehewa yaliyojaa kile kinachoaminika kuwa mchele na unga yakionekana kuvuka mpaka wa nchi kavu.
Mpango huu, unaoaminika kuwa wa thamani ya mamilioni ya dola, utakuza sio tu uchumi wa Pyongyang bali pia jeshi lake.
Urusi inaweza pia kuipatia Korea Kaskazini malighafi ili kuendelea kutengeneza makombora yake, au hata vifaa vya kijeshi kama vile ndege za kivita na msaada wa kiufundi wa kuboresha silaha zake za nyuklia.
Zaidi ya hayo, Kaskazini ina fursa ya kujaribu makombora yake mapya katika maeneo ya vita kwa mara ya kwanza. Na inaweza kuyaboresha.
‘Kwa kuwa sasa Pyongyang inazalisha silaha hizi kwa wingi, itataka kuziuza kwa nchi nyingi zaidi, na ikiwa makombora yanafaa kwa Urusi, yatafaa kwa wengine,’’ anasema Lewis.
Lewis anatabiri katika siku zijazo Korea Kaskazini itakuwa muuzaji mkuu wa makombora kwa China, Urusi na Iran.
Kufuatia shambulio la Iran dhidi ya Israel mwezi huu, Marekani ilisema ina wasiwasi mkubwa Korea Kaskazini inaweza kufanya kazi na Iran katika mipango yake ya nyuklia na makombora.
Spleeters anasema, ana matumaini na anafikiri kwa kufanya kazi na watengenezaji wa bidhaa wataweza kupunguza ugavi wa Korea Kaskazini.
Timu yake tayari imeweza kutambua na kufunga mtandao haramu kabla ya kukamilisha mauzo muhimu.
Lakini Lewis hajashawishika: "Tunaweza kuifanya biashara hiyo iwe ngumu au iwe ya gharama, lakini hakuna hata moja kati ya njia hizo itazuia Korea Kaskazini kutengeneza silaha hizi."
Akiongeza kuwa, ‘nchi za Magharibi zimeshindwa katika jaribio lake la kudhibiti hali hiyo mbaya. Sasa makombora yake sio tu chanzo cha heshima na nguvu ya kisiasa, lakini pia yanazalisha pesa nyingi.”
No comments:
Post a Comment