Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe. Nickson Simon John amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kupitia kikosi chake cha Ruvu JKT kwa kuendeleza sekta ya utalii nchini.
Mhe. Nickson ameyasema hayo wakati akizindua bustani ya wanyama pori walio wapole iliyopo katika kikosi cha Ruvu JKT kilichopo Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
Ameongeza kuwa Uzinduzi wa Bustani hiyo ni mwendelezo wa kuunga mkono Juhudi za Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizozifanya kupitia Filamu ya "The Royal Tour". Ambapo imeongeza idadi kubwa ya watalii nchini kutoka Mataifa mbalimbali.
Kwa upande wake Kamanda Kikosi Ruvu JKT Kanali Peter Mnyani amesema utunzaji wa mazingira ni moja ya jukumu la kikosi hivyo uwepo wa bustani ya wanyama pori hao utasaidia kutunza na kuendeleza misitu ya asili iliyopo kikosini hapo.
"Hapa ni stress free zone, wananchi wote wanakaribishwa kuja kuwalisha na kupiga nao picha wanyama hawa". Alisisitiza Kanali Mnyani.
Ruvu JKT Wildlife mpaka sasa ina wanyama mbalimbali wakiwemo Twiga, Pofu, Swala, Pundamilia na ndege wa kila aina.
Ukiwa kwenye bustani hiyo utapata huduma mbalimbali kama vile michezo ya watoto, mabwawa ya kuogelea kwa watoto na wakubwa.
Vile vile huduma za chakula, nyama choma pamoja vinywaji mbalimbali huduma ambazo zinapatikana kwa gharama nafuu.
Uzinduzi wa bustani ya wanyama pori Ruvu JKT ni mwendelezo wa uwepo wa bustani hizo katika vikosi vya JKT ambapo Kikosi cha Mbweni JKT nacho kimejikita katika mradi wa aina hiyo.
No comments:
Post a Comment