Habari kwamba Hamas imekubali kusimamisha mapigano ziliibua maandamano kuwataka viongozi wa Israel kufanya vivyo pia. |
Tangazo la Hamas la kusitisha mapigano limewashangaza waangalizi wengi na kubadilisha matarajio ya Israel ya kile ambacho kinaweza kutokea katika wiki chache zijazo.
Israel ilikuwa imefikilia kwamba Hamas haitakubali pendekezo la kusitisha mapigano ambalo Wamarekani waliliita "ukarimu wa kipekee".
Hapo awali, Israel iliwaonya Wapalestina kukimbilia upande wa mashariki wa Rafah, kwa sababu ya operesheni ya kijeshi inayokaribia.
Wamarekani wanapinga operesheni yoyote ya ardhini huko Rafah ambayo inaweza kutishia maisha ya raia.
Waziri wa ulinzi wa Israel, Yoav Gallant, alimweleza mwenzake wa Marekani kwamba hakuna njia mbadala - kwani Hamas ilikataa kila pendekezo la kusitishwa kwa mapigano kwa muda na kuachiliwa kwa mateka.
Wapatanishi kutoka Marekani, Misri na Qatar waliendelea kushinikiza kusitishwa kwa mapigano.
Mkuu wa CIA, William Burns, alitumia muda mwingi wa siku katika mikutano na waziri mkuu wa Qatar huko Doha, mji mkuu ambao pia ni ngome ya uongozi wa kisiasa wa Hamas.
Ilipofika jioni, Hamas ilipotangaza kuwa itakubali kusitisha mapigano , vyanzo vya Wapalestina vilidokeza kuwa inaweza kuwa tayari kwa mapatano ya muda mrefu.
Jibu la kwanza la Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu lilikuwa ni kusema kuwa Hamas "iko mbali na kutimiza matakwa ya Israel". Hata hivyo, ametuma wajumbe kujadili hilo.
Waziri mkuu netanyahu amebanwa kisiasa. Serikali yake ya mseto inategemea uungwaji mkono wa watu wenye itikadi za misingi ya utaifa wa Kiyahudi.
Wamedai wanataka kuwe na uvamizi kamili wa Rafah na kutishia kuiangusha serikali ikiwa hilo halitafanyika. Kusitishwa kwa mapigano kunamaanisha hakuna mapigano dhidi ya Rafah.
Wakati huo huo, familia na wanaowaunga mkono mateka wa Israel wamekuwa wakiandamana, wakifunga barabara kuu kuitaka Israel ikubali makubaliano ya kuwarejesha nyumbani mateka.
Wamarekani pia wanataka makubaliano. Uungaji mkono wa Rais Joe Biden kwa Israeli, hata kama jeshi lake liliua idadi kubwa ya raia wa Palestina, unaathiri uungwaji mkono wa kisiasa katika mwaka wa uchaguzi.
Hamas imemweka Bw Netanyahu chini ya shinikizo. Ikiwa Bw Biden atamshinikiza kukubali kusitishwa kwa mapigano itabidi achague kati ya kunusurika kwa serikali yake na uungwaji mkono muhimu ambao rais wa Marekani amempa tangu mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba.
Kusitishwa kwa mapigano pia kutamaanisha kuwa Israel haikupata "ushindi kamili" ambao waziri mkuu Netanyahu aliapa kuupata.
Mazungumzo zaidi, na maamuzi magumu, yanafuata.
No comments:
Post a Comment