SERIKALI YAPELEKA MAWASILIANO IGWAMADETE MANYONI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, May 16, 2024

SERIKALI YAPELEKA MAWASILIANO IGWAMADETE MANYONI


Na MwandishiWetu , Manyoni Singida.

NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi amemuelekeza mkandarasi anaejenga mnara wa mawasiliano katika kijiji cha Igwamadete Kata ya Iseke Wilayani Manyoni kuongeza nguvu kutoka vijiji 3 hadi vijiji 7 ili wananchi wa Maeneo hayo waweze kupata huduma ya mawasiliano.

Mhandisi Mahundi ametoa maelekezo hayo Mei 13,2024 alipofika katika eneo linapojengwa mnara huo na kujionea kazi inayoendelea ambapo amesema mradi huo umebakiza wiki mbili ili kukamilika.

“Leo tumekuja kukagua mnara unavyotekelezwa na furaha yangu kubwa ni kuwa, zimebaki wiki mbili ili mradi huu ukamilike na sisi tuanze kupangusa simu zetu popote pale ambapo tutakuwepo, hii ni furaha kubwa sana kwetu,

“Na tuna minara kumi na tano (15) tunaenda kuijenga kwenye kata zetu hizi na katika minara yote tunayoenda kuijenga huu ndio mnara mkubwa kuliko minara yote ambayo itaenda kusimama”amesema Mahundi

Mahundi amesema amefarijika kuona mnara wa mfano kutoka kwenye kijiji hiko na ndio mnara wa kwanza mrefu kujengwa kwenye Wilaya hiyo.

“Na kupitia ukubwa wa mnara huu tunajua mnaenda kupata mawasiliano mazuri, na katika kujiandikisha kwenye anuani za makazi”,amesema

“Na nataka niwaambie kuwa kuna paneli za kisasa zinaletwa kwahiyo tuwe walinzi sisi wenyewe, vile vifaa vikidumu visipoguswa guswa huduma ya mawasiliano itakuwa ya kudumu katika Wilaya hii”. Amesema Mahundi

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa UCSAF Pius Joseph amesema kutokana na urefu wa mnara huo ulivyojengwa kitaalam utawezesha makampuni mengine kuweza kuweka mitambo yao.

“Kampuni nyingine wanauwezo wa kuweka mitambo yao na kutoa huduma nyingine siyo Airtel peke yake kwa maana ya radio station na mitambo mengine”,amesema

Hata hivyo amesema mnara huo ni moja kati ya minara 758 ambayo imepangwa kujengwa.

“ Na mnara huu unajengwa na kampuni ya Airtel utakuwa na uwezo mkubwa wa kutoa huduma kwa kupiga simu na kupigiwa popote pale ulipo, na kasi yake itakuwa ni kasi ya 4G”, amesema

“Na pia mtaweza kuwasiliana kupitia whatsp, facebook, X na njia nyingine za mawasiliano, mradi huu utatatua changamoto hii ya mawasiliano kwa asilimia kubwa sana”. Amesema Pius
Nae Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki Dkt.Pius Chaya ameishukuru Serikali kwa kuendelea na jitihada za kupelekea mawasiliano katika kijiji hiko.

“Naishukuru sana Serikali kwa kutuona watu wa Igwamadete hapa mawasiliano ya simu ni mpaka kijiji cha pili kwahiyo kukamilika kwa mnara huu utatuwezesha sisi wakazi wa maeneo haya” amesema

No comments:

Post a Comment