|
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Bw. John Wanga, akizungumza wakati alipokutana na Timu ya Wataalam ya Wizara ya Fedha ambao walifika ofisini kujitambulisha kwa lengo la kuanza kutoa elimu ya huduma ndogo za fedha wilayani humo, ambapo kwa Mkoa wa Kagera watatoa elimu katika Wilaya nne za Bukoba, Missenyi, Muleba na Biharamulo. |
|
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Bw. John Wanga, (katikati), akiangalia filamu itakayotumika kwa wananchi wakati wa kutoa elimu ya huduma ndogo za fedha yenye mada mbalimbali ikiwemo elimu ya mikopo, akiba na uwekezaji. Kushoto ni Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya na Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Mary Mihigo. |
|
Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi. Mary Mihigo akichukua maoni kutoka kwa Wananchi wa Wilaya ya Missenyi baada ya kumalizika kwa semina iliyotolewa kwa njia ya filamu ikihusisha mada mbalimbali ikiwemo kujiandaa na maisha ya uzee na uwekezaji. |
|
Afisa Mwandamizi Uchambuzi Masuala ya Fedha kutoka Mamlaka ya Masoko na Mitaji na Dhamana (CMSA), Bi. Gladness Mollel, ekielezea umuhimu wa uwekezaji kwa wananchi wa Missenyi wakati wa semina iliyotolewa kwa wananchi hao iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri. |
|
Baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Missenyi walioshiriki semina ya elimu ya fedha wakifuatilia filamu yenye mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri. |
|
Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akifafanua jambo kwa baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Missenyi walioshiriki semina ya elimu ya fedha ambapo mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri. |
|
Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Missenyi walioshiriki semina ya elimu ya fedha baada ya kumalizika kwa semina iliyohusisha mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri. |
|
Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Bw. Flavian Nturwa, akifafanua jambo kwa baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Missenyi walioshiriki semina ya elimu ya fedha iliyokuwa na mada mbalimbali ikiwemo utunzaji wa akiba na mikopo iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Fedha) |
Na: Josephine Majula, WF- Kagera
Wananchi wametakiwa kushirikiana na Viongozi wa Serikali kuwafichua wamiliki wa Taasisi za Ukopeshaji fedha zisizo rasmi ili watakao bainika hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Rai hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Bw. John Wanga, alipokutana na Timu ya wataalamu ya Wizara ya Fedha ambao wanaendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wa mkoa wa Kagera katika Wilaya nne za Bukoba, Missenyi, Muleba na Biharamulo.
“Sisi kama viongozi wa Serikali tunatakiwa tuendelee kushirikiana na Wananchi kuwakemea watoa huduma wasio na nia njema kwa Taifa wanaojali maslahi yao binafsi”, alisema Bw. Wanga.
Alisema kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kwenda kinyume na maelekezo waliyopewa na Benki Kuu ya Tanzania kabla hawajapatiwa leseni ya kuendesha shughuli za utoaji mikopo.
Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi, Bw. Flavian Nturwa, alisema kuwa ni wajibu wa Waratibu wote wa Huduma Ndogo za Fedha kuhakikisha wanatoa elimu kwa wananchi katika ngazi zote ili wawe na uelewa mpana wa masuala ya fedha.
“Tutahakikisha tunafanya mikutano ya mara kwa mara kwa wananchi wa pande zote, watoa mikopo na wapokeaji ili wawe na uelewa wa pamoja hususan elimu ya mikataba ili kuepuka kusaini mikataba yenye masharti magumu”, alisema Bw. Nturwa.
Naye mtoa Huduma za Mikopo Bw. Salehe Hamisi, alisema kuwa elimu itolewe kuhusu utaratibu wa kusajili Taasisi za Fedha ili Wafanyabiashara waweze kujisajili kwa wingi na kutambulika rasmi.
Naye Afisa Usimamizi wa Fedha Idara ya Uendelezaji Sekta ya Fedha Wizara ya Fedha, Bi.Mary Mihigo, aliwasisitiza wananchi kuwa na nidhamu ya matumizi ya fedha na kutunza akiba.
Wizara ya Fedha inaendelea na zoezi la utoaji elimu kwa wananchi kuhusu huduma ndogo za fedha ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na elimu ya huduma ndogo za fedha.
No comments:
Post a Comment