TANROADS YAENDELEA NA KAZI YA UPANUZI WA BARABARA YA UBUNGO - KIMARA KUPUNGUZA MSONGAMANO. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, May 31, 2024

TANROADS YAENDELEA NA KAZI YA UPANUZI WA BARABARA YA UBUNGO - KIMARA KUPUNGUZA MSONGAMANO.


Serikali kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa barabara kutoka Ubungo mpaka Kimara ili kupunguza msongamano wa magari katika barabara hiyo Jijini Dar-es-Salaam.

Hayo yameelezwa na Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mha. Mohamed Besta alipozungumza na kituo cha Runinga cha ITV katika kipindi cha Kumekucha Mei 31, 2024 ambapo ameeleza kuwa mradi wa upanuzi wa Barabara hiyo unatekelezwa chini ya mpango wa Dar es Salaam Urban Transport Improvement Project (DUTP) ambao unafadhiliwa na Benki ya Dunia.

"Tumepata fedha kutoka Benki ya Dunia kuongeza upana wa barabara kutoka Ubungo mpaka Kimara ili kuwe na njia tatu kila upande na hivyo kupunguza msongamano hasa nyakati za jioni, nafahamu adha ambayo Wananchi wanapitia, sasa hivi mkandarasi yuko site ili kuanza kazi hii, kazi unayoiona inaendelea ni kusafisha pembezeni mwa barabara ili kupata eneo la kuweza kujenga njia mpya kwa ajili ya kupunguza msongamano’’ amesema Mha. Besta

Aidha, ameeleza kuwa ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa kwa miezi 24, hautahusisha kubomolewa kwa nyumba au makazi ya watu kwani tayari kazi hiyo ilishafanyika huko nyuma na kutokana na hali ilivyo kutakuwa na ujenzi wa barabara peke yake.

Kuhusu kumalizia kazi ya kusimika taa katika Barabara ya Kimara – Kibaha; Mha. Besta amesema taa zipo katika sehemu ya mkataba katika ule mradi, timu ya Wataalam kutoka TANROADS pamoja na timu ya Mkandarasi wameshafanya ziara ya kwenda Japan kwa ajili ya kununua taa hizo, hatuwezi kununua taa tu na kuziweka lazima uende kiwandani na lazima kufanya majaribio kwamba hii taa itadumu na ipo katika viwango vinavyotakiwa.

Ameongeza kuwa Taa hizo zinakuja kuanzia mwezi wa sita mwaka huu na zitaanza kuwekwa na Mkandarasi ili kukamilisha mradi huo kutoka Kimara mpaka Kibaha.

No comments:

Post a Comment