Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imesema itaweka taa za kuongoza magari Tarime Mjini katika eneo la Jembe na Nyundo ili kupunguza ajali za barabarani zinazotokea mara kwa mara kwenye eneo hilo.
Hayo yameelezwa leo Mei 17,2024 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Esther Matiko aliyeuliza Je, lini Serikali itaweka taa za kuongoza magari pamoja na taa za barabarani katika Mji wa Tarime kwa kuwa Mji huo unapitisha magari mengi ya abiria na biashara.
Eng. Kasekenya amesema katika mwaka wa fedha 2022/23 Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mara, iliweka jumla ya taa mia moja thelathini na tatu (133) katika Mji wa Tarime kuanzia eneo la Buhemba hadi Tarime Hill (eneo la Magere).
"Katika mradi wa Ujenzi wa Barabara unaoendelea kuanzia Tarime Mjini hadi Mogabiri yenye urefu wa kilometa 9.3 utajumuisha pia uwekaji wa taa za barabarani kwa sababu tumeshaweka kwenye mpango na katika miradi yote tunayotekeleza tutajumuisha uwekaji wa taa", amesema Eng. Kasekenya.
No comments:
Post a Comment