KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA), Dingani Banda wameweka mikakati ya kuimarisha utendaji kazi wa mpaka wa Tanzania na Zambia, Tunduma ili kuwahudumia kwa ufanisi wasafiri na wasafirishaji kutoka pande zote.
Akizungumza na waandishi wa.habari jana Kamishna Kidata alisema wamejipanga kuimarisha mpaka wa kuingia Tanzania na kwenda Zambia.
Alisema wataalamu kutoka Tanzania na Zambia wako imara katika utendaji katika kazi zao za kila siku kwa wafanya biasharaena jamii kwa ujumla.
“Tumekubaliana kwa pamoja kuimarisha utendaji kazi wa mpaka huu kwa sababu ni muhimu kwa maslahi ya nchi zetu na tunaimarisha mifumo ya forodha, ufanisi na uwajibikaji katika kurahisisha mifumo ya uvushaji mizigo na bidhaa na kuzuia mianya yote ya magendo”, alisema Kidata.
Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zambia (ZRA), Dingani Banda amepongeza ujio wa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Alphayo Kidata ambaye aliongozana na timu ya viongozi mbalimbali kutoka TRA na kuahidi kuwa yeye na timu yake watayafanyia kazi maazimio mbalimbali waliyokubaliana katika mkutano huo na kupanga tena siku nyingine ya kukutana na kupeana mrejesho.
Aidha Makamishna hao wamejadili na kukubaliana kuimarisha mikakati ya pamoja ya kuboresha mpaka wa Kasesya uliopo wilayani Kalambo mkoani Rukwa ambao utapunguza msongamano wa magari katika mpaka wa Tunduma.
“Tumekubaliana kuimarisha mpaka wa Kasesya ambao kwetu ni wa kimkakati na nimepita jana kujionea mwenyewe hali ilivyo pale kwa sababu ni fursa kwetu”, aliongeza Kidata.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Afisa Mfawidhi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kassim Mhando makusanyo ya kodi mpakani hapo katika kipindi cha miezi 10 yaani kuanzia mwezi wa Julai, 2023 hadi Aprili, 2024 TRA TRA ilifanikiwa kukusanya jumla ya shilingi bilioni 122.3 kati ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 120.5 sawa na ufanisi wa asilimia 101.5.
Pia aliongeza kuwa, moja ya manufaa ambayo nchi ya Tanzania na Zambia inanufaika na mpaka huo wa Tunduma ni wastani wa uvushaji magari kwa siku ambao ni zaidi ya magari elfu moja yanayotoka kuingia Tanzania na hiyo imetokana na matumizi thabiti ya skana mpya ya kisasa inayoweza kuvusha magari mengi kwa muda mfupi na kuepusha foleni.
“Moja ya faida zinazopatikana katika mpaka huu ni idadi ya mizigo inayoenda nje ya nchi inaongezeka mwaka hadi mwaka hali ambayo inapelekea mapato kuongezeka”, alisema Mhando.
Mhando ameeleza pia, hali ya udhibiti wa magendo mpakani hapo kupitia Idara ya Forodha katika Kitengo cha Udhibiti na Ushurutishaji imekua nzuri kwasababu kitengo hicho kinafanya doria mbalimbali na kimekua kikikamata magendo, kwa mfano kwa mwaka huu wa fedha kimekamata jumla ya tani 160 za vipodozi ambavyo vimethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa havifai kwa matumizi ya binadamu.
Makamishna wote wawili wamekubaliana kwa pamoja kukutana tena mapema mwezi Agosti mwaka huu kwa ajili ya mrejesho wa mambo waliyokubaliana katika kikao walichofanya mjini Tunduma.
No comments:
Post a Comment