Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Wizara ya Ujenzi na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), wametoa mafunzo ya aina mbalimbali kwa watumishi wa mizani katika mikoa sita ya Kanda ya Ziwa ili kuhakikisha sheria na kanuni zinazosimamia mizani nchini zinazingatiwa kikamilifu.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mhandisi Leonard Saukwa kutoka Wizara ya Ujenzi amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo watumishi wa mizani ili waweze kufanya kazi zao kwa kufuata sheria na hivyo kuleta tija na ufanisi katika vituo vyao vya kazi.
Mha. Saukwa amezungumzia umuhimu kwa watumishi wa mizani kuwaelimisha wasafirishaji njia za kuomba vibali vya kusafirisha mizigo isiyoyakawaida (abrnomal loads), ili kuwezesha usafirishaji huo kufanyika kwa haraka na wakati.
Mafunzo hayo yatawawezesha washiriki kuelewa utekelezaji wa sheria ya Jumuia ya Afrika Mashariki iliyoanza kutumika mwaka 2019 mwezi Machi ya namna ya udhibiti wa mizigo na kuzilinda barabara ziwe salama wakati wote, ambapo kwa sasa elimu inayotolewa imewezesha wasafirishaji wengi kufuata sheria na hivyo kusababisha idadi ya magari yanayozidisha uzito kupungua.
Kwa upande wake Afisa Rasilimali Watu Mwandamizi wa TANROADS Makao Makuu, Bi. Scolastica Mgaya amewaelekeza washiriki kufuata kanuni za kudumu katika utumishi wa umma hususan kanuni F yenye suala la tabia na mwenendo wa maadili na taratibu za kinidhamu.
Amesisitiza kufanyakazi kwa bidii na ubunifu ili kuiwezesha serikali kupata faida na hivyo kufikia lengo la kulinda miundombinu yake ya barabara na kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.
Mkutano wa semina elekezi kwa watumishi wa mizani kanda ya ziwa unaoendelea jijini Mwanza unahusisha wataalam toka mikoa ya Mwanza ,Shinyanga, Simiyu,Mara, Geita na Kagera lengo likiwa ni kuwajengea uwezo watumishi hao ili kutoa huduma bora kwa wasafirishaji na kuleta tija katika sekta ya usafirishaji nchini.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO SERIKALINI TANROADS
No comments:
Post a Comment