Na Carlos Claudio, Dodoma.
Kamati ya mpito ya kuratibu uchaguzi wa baraza la mashirika yasiyo ya kiserikali NaCoNG0 imetangaza matokeo ya uchaguzi ngazi ya mkoa ambao ulifanyika Juni 11, 2024.
Hayo yameelezwa leo Juni 15, 2024 jijini Dodoma na mwenyekiti kamati ya mpito ya kuratibu uchaguzi wa baraza la taifa la NGOs Christina Ruhinda alipokutana na waandishi wa habari katika ofisi ya chama hicho ambapo amesema wajumbe 30 wa baraza la NaCoNGO walipatikana huku wajumbe 26 walishinda kutoka katika ngazi ya mkoa, wajumbe 4 kutoka makundi maalum (wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya kiserikali ya watoto, vijana, watu wenye ulemavu na za kimataifa).
Amesema uchaguzi huo ulikuwa wa uwazi, uhuru, haki na amani ukifuata sheria za nchi, kanuni na miongozo ya mashirika yasiyo ya kiserikali huku wasimamizi walikuwa wawakilishi wa mashirika yasiyo ya kiserikali na waangalizi walikuwa wasajili wasaidizi ngazi ya mkoa.
“Jumla ya wajumbe 288 kutoka wilaya zote Tanzania bara ambao ni wawakilishi wa baraza katika ngazi ya wilaya na wapiga kura halali wanaume 214 na wanawake 74 walishiriki uchaguzi katika ngazi ya mkoa, kati ya wajumbe 288, wajumbe 125 walijitokeza kugombea nafasi ya ujumbe wa baraza ngazi ya mkoa, na kati yao waliokidhi vigezo vya kugombea walikuwa wajumbe 77, yaani wanaume 66 na wanawake 11,”
“Kamati ya mpito ya kuratibu uchaguzi wa NaCoNGO inawashukuru mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yaliyojitokeza kupiga kura na kugombea, wasimamizi na waangalizi wa uchaguzi kwa kujitolea kwa hali na mali kufanikisha uchaguzi huu,” amesema Ruhinda.
Aidha kamati hiyo inawatangazia wajumbe 30 wa baraza ngazi ya mkoa kuwa kutakuwa na uchaguzi wa viongozi wa baraza la NaCoNGO ngazi ya kitaifa utakaofanyika Dodoma Juni 25, 2024 huku nafasi zinazogombewa katika ngazi ya taifa ikiwa mwenyekiti, katibu mkuu, mweka hazina, wawakilishi wa kwenye bodi, mwenyekiti wa kamati ndogo nne za maadili zikiwa fedha, maendeleo ya uwezo pamoja na mawasiliano.
Ruhinda amesema mwombaji wa nafasi ya uongozi wa baraza ngazi ya taifa anatakiwa kujaza fomu ya maombi inayopatikana kwenye tovuti ya baraza www.nacongo.or.tz na kuiwasilisha kupitia barua pepe uchaguzinacongo@gmail.com huku fomu hiyo ikiambatanishwa na nakala ya kiapo cha kiongozi katika ngazi ya Mkoa au makundi maalum au mashirika ya kimataifa, vyeti vya taaluma, mafunzo mbalimbali, maelezo binafsi ya mgombea (CV) pamoja na cheti cha shirika analotoka mgombea ambayo yatawasilishwa yakiwa na viambatanisho vyake vyote kama nyaraka moja katika mfumo wa PDF.
Ameongeza kuwa fomu zitaanza kupakuliwa na kuwasilishwa kwa kamati kuanzia Juni 17 hadi Juni 19, 2024 huku kamati hiyo itafanya uchambuzi wa fomu za maombi ya kugombea nafasi za uongozi na kupendekeza wagombea wasiozidi 3 katika kila nafasi.
Amesema Juni 25, 2024 kutakuwa na mkutano wa baraza kwa ajili ya uchaguzi wa viongozi wa baraza katika ngazi ya Taifa pia katika mkutano huo wagombea wote watanadi sera zao mbele ya wajumbe kabla ya kupigiwa Kura.
“Wagombea wasiozidi 3 waliopendekezwa katika kila nafasi watapigiwa kura na mgombea mwenye kura nyingi ndiye atatangazwa kuwa mshindi kwa nafasi husika, kwa nafasi ambazo mgombea aliyejitokeza ni mmoja pia atapigiwa kura na Wajumbe wa baraza wagombea walioshinda katika nafasi mbalimbali za uongozi wataapishwa mbele ya wakili au hakimu aliyeandaliwa kwa ajili ya kazi hiyo.”
Ruhinda ameongeza kuwa, “tarehe 26,Juni 2024 kutafanyika uzinduzi rasmi wa baraza la taifa la mashirika yasiyo ya kiserikali litakalozinduliwa rasmi na waziri mwenye dhamana ya mashirika yasiyo ya kiserikali au kiongozi yoyote mwandamizi atakayeteuliwa na waziri kutekeleza majukumu hayo kwa niaba yake.”
Sambamba na hayo kamati hiyo imetoa wito kwa wajumbe wote 30 kushiriki kikamilifu katika mkutano wa kwanza wa baraza la kitaifa la mashirika yasiyo ya kiserikali utakaofanya uchaguzi wa baraza ngazi ya taifa Juni 25, 2024 jijini Dodoma pamoja na kamati hiyo kutoa taarifa juu ya kuanza kwa mchakato wa uchaguzi ngazi ya kitaifa.
No comments:
Post a Comment