THRDC NA TRA WAZINDUA KITABU CHA MWONGOZO KUHUSU KODI KWA MASHIRIKA YASIYOJIENDESHA KWA FAIDA TANZANIA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, June 3, 2024

THRDC NA TRA WAZINDUA KITABU CHA MWONGOZO KUHUSU KODI KWA MASHIRIKA YASIYOJIENDESHA KWA FAIDA TANZANIA

Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw.Onesmo Ole Ngurumwa,(wa pili kutoka kulia) akiwa na Kamishna wa kodi za ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Bw. Alfred Mregi (wa pili kutoka kushoto) wakionesha kitabu cha Mwongozo kuhusu kodi kwa Mashirika Yasiyojiendesha kwa Faida Tanzania kilichozinduliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kamishna wa kodi za ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Bw. Alfred Mregi,akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha kuhusu kodi kwa Mashirika Yasiyojiendesha kwa Faida Tanzania kilichozinduliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw.Onesmo Ole Ngurumwa,akizungumza wakati wa uzinduzi wa kitabu cha kuhusu kodi kwa Mashirika Yasiyojiendesha kwa Faida Tanzania kilichozinduliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Na.Mwandishi Wetu - DODOMA


MTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamezindua mwongozo kuhusu kodi kwa Mashirika Yasiyojiendesha kwa Faida Tanzania.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo jijini Dodoma Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Bw.Onesmo Ole Ngurumwa,amesema kuwa wazo la kuandaa na kuchapisha mwongozo wa kwanza uliletwa wakati wa mkutano wa wakurugenzi wa AZAKi uliofanyika mkoani Mwanza 2019 na ilipokelewa vyema na TRA na AZAKi nchini kote.

Amesema kuwa bado kuna faini na riba ambazo huwa zinatozwa na TRA hata kama asasi inakuwa haina mradi unaotekelezwa kwa sababu tu imeshaingizwa kwenye mfumo wa kulipa kodi.

“Kwa mfano unakuta asasi haijapata mradi kwa miaka mitatu mfululizo lakini kule TRA riba na faini zinaendelea kusoma matokeo yake asasi zinakuwa na madeni makubwa ya kodi asiyolipika na hivyo kurudisha nyuma malengo yao ya kuhudumia jamii,” amesema Ole Ngurumwa.

Amesema asasi hizo zina mchango mkubwa kwa jamii kwani zinachangia asilimia 40 ya huduma kwenye sekta ya elimu huku kwenye sekta ya afya zikichangia asilimia 50 na kwenye sekta nyingine kama maji, miundombinu, kilimo na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake Kamishna wa kodi za ndani kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)Bw. Alfred Mregi amesema kuwa dhamira ya TRA ni kufanya kazi na wadau wote katika kuhakikisha kwamba kila mtu anatimiza wajibu wake katika kulipa kodi.


“TRA inatambua jukumu la AZAKi katika kulipa kodi zote za kisheria, niwahakikishie kuwa tutaendelea kufanya kazi pamoja kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii,’’ alisema.


Pia amesema kuwa kiwango cha uelewa wa masuala ya kodi kimeendelea kukua kwa Mashirika Yasiyojiendesha kwa Faida hapa nchini.

“Taarifa zetu zinaonesha kuwa kiwango cha uelewa wa masuala ya kodi kimeendelea kukua katika kundi hilo kutokana na na uwepo wa mafunzo ya kodi kwa AZAKI na matumizi ya kijarida kwa muda mrefu,” amesema

Aidha amesema kuwa asasi nyingi za kiraia zina changamoto katika kutekeleza sheria kodi.

“TRA itaendelea kushirikiana a THRDC na wadau wake wengine kuhakikisha kuwa makundi yote ya AZAKI yanafikiwa,” amesema

Naye mjumbe wa Baraza la Taifa la Asasi za kiraia (NaCongo), Bi.Penina Manyanki amesema kitabu hicho kinekuja wakati muafaka kwani hata wale ambao hawajasomea sheria wataweza kuelewa kodi zinazotakiwa kulipwa badala ya kuwatafuta wanasheria wawatafsirie sheria hizo.


“Kitabu hicho kitaondoa malalamiko ya asasi za kiraia kwani wengi walikuwa hawajui kodi wanazotakiwa kulipa na mwisho wa siku walikuwa wanajikuta wana madeni makubwa ya kodiambazo walikuwa hawajui yanatoka wapi.”amesema

No comments:

Post a Comment