Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama ameagiza wataalamu wote waliopangiwa na watakaopangiwa kufanya kazi katika chumba cha ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga na tahadhari ya mapema kuhakikisha kuwa shughuli zilizopangwa kufanyika zinatekelezwa kwa ufanisi na kunakuwepo na mwendelezo ili kuhakikisha taarifa za tahadhari za mapema zinawafikia walengwa kwa wakati hasa wanajamii na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga.
Mhe. Mhagama ameyasema hayo leo Juni 14, 2024 jijini Dodoma, wakati wa uzinduzi wa chumba cha ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga na tahadhari ya mapema katika kituo cha taifa cha operesheni na mawasiliano ya dharura.
Amesema uwepo wa chumba hiko iwe ni fursa kwawadau wote katika kuboresha hatua mbalimbali za kuzuia, kujiandaa,kukabiliana na maafa na kurejesha hali baada ya maafa kutokea katika maeneo yote nchini.
“Nimejulishwa kuwa wataalamu 27 wamepatiwa mafunzo ya kina kuhusu mifumo itakayotumika kwenye chumba cha ufuatiliaji wa majanga na utoaji wa tahadhari za awali ambapo kati ya hao, 8 kutoka ofisi ya Waziri Mkuu, 14 kutoka Wizara ya Maji na 5 kutoka malmaka ya Hali ya Hewa Tanzania vilevile nimejulishwa kuwa wataalamu sita 6 kati ya waliopata mafunzo wameainishwa kuwa watatekeleza shughuli za ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga na utoaji wa tahadhari za mapema na uchukuaji wa hatua za haraka katika chumba hiki,”
“Nimejulishwa kuwa chumba hiki kimefungwa vifaa mbalimbali vya TEHAMA pamoja na mifumo mbalimbali ya kufuatilia mwenendo wa majanga na tahadhari ya mapema ikijumuisha jukwaa la ki-eletroniki la myDEWETRA, vilevile nimefahamishwa kuwa Jukwaa hili la ki-eletroniki la myDEWETRA limeunganisha taarifa za kijiografia kwa ajili ya uchambuzi wa utabiri wa hali ya hewa na haidrolojia hatarishi ya mafuriko, ukame, vimbunga, Tsunami, upepo mkali na majanga mengine ili kuweza kufanya tathmini ya madhara na kutoa tahadhari ya mapema kwa wakati na eneo husika,” amesema Mhagama.
Aidha amesema kuwa kupitia majanga mbalimbali yaliyotokea nchini na athari zilizotokea, serikali imeona umuhimu wa kuendelea kuimarisha mifumo ya tahadhari za awali na ufuatiliaji wa majanga kwa kuanzisha chumba chenye vifaa na mifumo ya kisasa kwa ajili ufuatiliaji wa mwenendo wa majanga mbalimbali na uchukuaji wa hatua za mapema.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, ofisi ya waziri mkuu, sera bunge na uratibu Dkt. Jim Yonazi amesema shughuli za menejimenti na uratibu wa maafa nchini zinatekelezwa kwa kuzingatia sheria ya usimamizi wa maafa na.6 ya mwaka 2022 pamoja na kanuni zake za usimamizi wa maafa za mwaka 2022.
Amesema sheria hiyo katika kifungu cha 4(1) imeipa ofisi ya Waziri Mkuu jukumu la kuratibu na kusimamia shughuli za maafa nchini pamoja na kuwa na mifumo ya tahadhari ya mapema na ufuatiliaji wa majanga itakayojumuisha sekta zote na kuwa kiungo kati ya taasisi mbalimbali zinazotoa huduma ya tahadhari kupitia Kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura.
“Kwa kuzingatia umuhimu wa uanzishwaji wa chumba hiki katika kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura, ofisi ya Waziri Mkuu ilitekeleza jukumu la kuratibu ushirikiano na ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza madhara ya maafa katika Kanda ya Afrika na taasisi CIMA Research Foundation ya Italia katika uanzishwaji wa chumba hiki cha ufuatiliaji wa majanga na uundaji wa jukwaa la kielektroniki lijulikanalo ka myDEWATRA,” amesema Yonazi.
Nae raisi wa CIMA foundation Luca Ferraris amesema wameanza na wasifu wa hatari ya mafuriko na ukame kwa nchi 16 katika nchi ikiwemo Tanzania, ikiwa mwaka wa 2018 ambapo UNDRR ilishirikisha na CIMA, kama taasisi ya kisayansi kwa ajili ya kukadiria athari za mafuriko na ukame chini ya makadirio ya sasa na ya baadaye ya hali ya hewa, kijamii, kiuchumi na kuwasilisha matokeo hayo kwa watunga sera.
Ameongeza kuwa tafiti zingine za hivi majuzi ambazo zilitengenezwa na kituo cha ufuatiliaji wa uhamisho wa ndani cha UN zilionyesha kuwa zaidi ya watu elfu 50 wako katika hatari ya kuhama kila mwaka.
Uanzishwaji wa chumba hiko muhimu cha ufuatiliaji wa majanga na tahadhari ya mapema umefanikiwa kutokana na mradi ulioanzishwa na ofisi ya umoja wa mataifa ya kupunguza madhara ya maafa katika kanda ya Afrika na kufadhiliwa na serikali ya nchi ya Italia kupitia shirika la maendeleo la Italia (Italian Agency for Development Cooperation) ambapo Taasisi ya CIMA Research Foundation ya Italia imesadia kutoa utaalamu wa utekelezaji wa shughuli zote.
No comments:
Post a Comment