Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa amezindua kampeni ya nishati safi ya kupikia Wilayani Karagwe kwa kugawa mitungi ya gesi 300 kwa Wanawake Wajasiliamali na wenye mahitaji maalum ikiwa ni mwendelezo wa kuunga mkono Agenda ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya matumizi ya nishati safi.
Bashungwa amezindua kampeni hiyo leo Julai 04, 2024 Wilayani Karagwe, Mkoani Kagera ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024 - 2034 ambao unalenga kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ya Watanzania wanaotumia nishati hiyo.
“Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatambua changamoto mnazopitia akina mama wakitanzania majumbani katika shughuli mbalimbali ikiwemo za upishi na ndio maana amekuja na mkakati wa kuongeza matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia katika maeneo yote ya nchi”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa mkakati wa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia utakuwa endelevu ambapo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali na kuhakikisha Wilaya ya Karagwe inakuwa kinara wa matumizi ya nishati safi na salama.
Bashungwa ametoa pongezi za dhati kwa uongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya Wilaya, Waheshimiwa madiwani, uongozi wa Halmashauri ya Karagwe pamoja na Wakuu wa Idara na watumishi wote kwa kuungana pamoja katika utoaji elimu ya kampeni hiyo ya nishati safi na salama ya kupikia Wilayani Karagwe.
Aidha, Bashungwa ametumia nafasi hiyo kueleza juhudi mbalimbali za Serikali katika utekelezaji wa miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na Serikali katika Sekta ya afya, elimu, miundombinu ya barabara na maji katika kata zote za Wilaya ya Karagwe.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Karagwe, Rasul Shandala amempongeza Waziri Bashungwa kwa namna ambavyo amejipanga kuleta maendeleo katika Wilaya hiyo na kueleza kuwa maendeleo ya Karagwe yanakuwa kwa kasi kutokana na wito wake kwa wanakaragwe na amekuwa na ushirikiano na viongozi wa ngazi zote na hivyo kufanya Wilaya hiyo kuwa kieleezo chema na wa kuigwa kwa Mkoa wa Kagera.
Akiwasilisha Risala, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Dkt. Amon Mkogya ameeleza kuwa takwimu zinaonesha wananchi wa Wilaya ya Karagwe wanatumia nishati ya kuni na mkaa kupikia ambapo vyanzo hivyo vinapelekea uharibifu na uchafuzi wa mazingira na hali ya hewa na kuathiri viumbe hai kiafya.
No comments:
Post a Comment