Na Mwandishi Wetu WHMTH
Serikali yakamilisha Majadiliano kati yake na Kampuni ya Viettel Global Joint Stock ya Vietnam kuhusu utekelezaji wa mkataba wa ufikishaji mawasiliano ikiwepo ujenzi wa miundombinu ya mkongo ulioingiwa mnamo mwaka 2014.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa vikao hivyo vya majadiliano tarehe 19 Julai, 2024, Mwenyekiti wa Timu ya Majadiliano ya Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bw. Adolf Ndunguru amesema majadiliano yaliyokuwa yakiendelea kuhusu utekelezaji wa mkataba huo yamekamilika.
Aidha, Mwenyekiti ameeleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itaendelea kushirikiana na kampuni hiyo na kuhakikisha uwepo mazingira mazuri na wezeshi katika Sekta ya Mawasiliano.
“Leo tumehitimisha majadiliano na kampuni ya Viettel kuhusu mgogoro uliokuwepo kwa muda mrefu kwenye sekta ya mawasiliano, na majadiliano haya yamekamilika kwa kila upande kuridhika na hatua iliyofikiwa”, amesema Bw. Ndunguru.
Nae kiongozi wa Timu ya Majadiliano wa Kampuni ya Viettel Global Joint Stock Investment Bw. Phung Van Cuong ameishukuru Serikali ya Tanzania, Timu ya Serikali ya Majadiliano na Timu ya Wataalam ya Serikali kwa kukamilisha majadiliano haya na kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.
“Kwa niaba ya Kampuni ya Viettel Global tunasema asante sana kwa Serikali ya Tanzania kwa kusaidia uwekezaji wetu, sisi tunaahidi kuendelea kuwekeza zaidi katika sekta ya mawasiliano, tunashukuru sana” amesema Bw. Phung Van Cuong.
No comments:
Post a Comment