MAKALA
Na Wizara ya Madini
Sekta ya Madini ni moja ya nguzo muhimu za uchumi wa Tanzania. Pamoja na mchango mkubwa unaotolewa na Migodi mikubwa inayomilikiwa na Kampuni za ndani na nje ya Taifa sambamba na zile za ubia baina ya Serikali na kampuni za kigeni. Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini bado ni tija kubwa katika maendeleo ya sekta hii.
Pamoja na kwamba wachimbaji wadogo wanatumia nyenzo duni za kiteknolojia isiyo ya kisasa sambamba na changamoto ya mitaji midogo bado wana mchango mkubwa wa kuchangia pato la taifa, kutoa ajira na kuboresha maisha ya Watanzania wengi.
Katika Makala hii tutachambua mchango wa wachimbaji wadogo katika Sekta ya Madini nchini Tanzania, na hatua zinazochukuliwa hadi sasa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kuwezesha kundi hili muhimu kukua.
Mchango wa Wachimbaji Wadogo Katika Sekta ya Madini Hapa Nchini
Katika miaka ya hivi karibuni, mchango wa wachimbaji wadogo kwenye mapato ya Sekta ya Madini umekuwa ukikua kwa kasi. Takwimu kutoka Wizara ya Madini zinaonyesha kuwa mchango wa wachimbaji wadogo umeongezeka kutoka asilimia tano (5%) kabla ya marekebisho ya Sheria ya Madini Mwaka 2017 hadi kufikia takribani asilimia arobaini (40%) katika mwaka wa fedha 2022/2023. Ongezeko hili ni ishara ya wazi ya umuhimu wao katika sekta hii. Wachimbaji wadogo wameweza kutoa mchango mkubwa katika uzalishaji wa madini mbalimbali kama vile dhahabu, Tanzanite, na vito vingine, na hivyo maduhuli ya Serikali kuongezeka kwa kasi kubwa .
Ajira na Maendeleo ya Kijamii Kutokana na Wachimbaji Wadogo
Wachimbaji wadogo wa madini wametoa ajira kwa maelfu ya Watanzania, hususan katika maeneo ya vijijini ambako fursa za ajira ni chache sana. Ajira hizi zinawasaidia watu wa jinsi tofauti kupata kipato cha kujikimu na kuboresha hali zao za maisha. Pamoja na ajira, uchimbaji mdogo wa madini unachangia katika maendeleo ya jamii kwa kuchangia huduma za kijamii kama vile shule, vituo vya afya, na miundombinu mingine muhimu. Maeneo mengi yenye shughuli za uchimbaji mdogo wa madini yamekuwa na maendeleo ya kasi katika utoaji wa huduma za kijamii kutokana na mchango wa moja kwa moja wa wachimbaji wadogo.
Utoaji wa Leseni kwa Wachimbaji Wadogo na Kudhibiti Utoroshaji wa Madini
Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo kupitia utoaji wa leseni na kudhibiti utoroshaji wa madini. Ongezeko la utoaji wa leseni za madini kutoka leseni 5,094 katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 hadi leseni 10,067 katika kipindi kama hicho kuanzia Julai 2023 hadi Machi 2024 kati ya hizo, Leseni 6,934 ni za Uchimbaji Mdogo (PMLs).
Kwa upande mwingine, kuanzishwa kwa Masoko ya Madini nchini Tanzania kumesaidia kudhibiti utoroshaji wa madini na kuongeza uwazi katika Sekta ya Madini ambapo hadi sasa kuna jumla ya Masoko 42 na Vituo 100 vidogo vya ununuzi wa madin hapa nchini.
Masoko hayo yamesaidia kuweka mifumo ya kufuatilia na kusimamia biashara ya madini, ikiwemo teknolojia za kidijitali ambazo zinasaidia kurekodi taarifa za madini kutoka kwa wachimbaji hadi kwa wanunuzi,
Pia, kuanzishwa kwa Masoko hayo yamesaidia kudhibiti bei kwa kutoa bei elekezi ambazo ni shindani na za haki, sawa na soko la dunia hivyo kupunguza hamasa ya watu kutorosha madini kwa nia ya kuuza kwa bei ya juu zaidi kwenye soko la magendo. Vilevile Masoko hayo yamesaidia kuongeza mapato ya serikali kupitia tozo na ada mbalimbali zinazotozwa kwenye masoko haya
Juhudi za Ushirikiano Baina ya Wachimbaji Wadogo na Taasisi za Fedha
Changamoto kubwa inayowakabili wachimbaji wadogo ni ukosefu wa mitaji na teknolojia ya kisasa. Serikali, kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), imechukua hatua za kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo na mitaji kwa kushirikiana na taasisi za fedha. Makubaliano kati ya STAMICO na benki kama CRDB, KCB, na NMB yamekuwa chachu kwa taasisi za fedha na kujenga imani kwa wachimbaji wadogo. Ushirikiano huu umewawezesha wachimbaji wadogo kupata mikopo kwa riba nafuu na hivyo kuweza kununua vifaa vya kisasa na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi zaidi.
Kwa mfano, katika kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024, jumla ya shilingi bilioni 187 zilikopeshwa kwa wachimbaji wadogo, ikilinganishwa na shilingi bilioni 145 zilizokopeshwa mwaka 2022.
Mafunzo kwa Wachimbaji Wadogo na Maendeleo ya Teknolojia
STAMICO imeandaa mpango wa kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo kwa kuzunguka nchi nzima. Mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wachimbaji wadogo kutumia teknolojia bora na za kisasa ili kuongeza tija katika uchimbaji wao. Ushirikiano na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) umesaidia pia katika kupata taarifa muhimu za kijiolojia zinazowawezesha wachimbaji wadogo kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Kupitia Vision 2030: Madini ni Maisha na Utajiri, GST imekusudia kutumia teknolojia ya kisasa kufanya utafiti wa kijiofizikia (High Resolution Geophyiscal Survey) kwa kutumia ndege nyuki (drones) zisizo na rubani katika utafiti wa madini ili kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata taarifa kina za mashapo kwenye maeneo yenye madini.
Changamoto Zinazowakabili Wachimbaji Wadogo
Licha ya mchango mkubwa unaoendelea kutolewa na Sekta mdogo ya uchimbaji mdogo nchini unakabiliwa na changamoto nying ikiwa ni Ukosefu wa mitaji na teknolojia ya kisasa. Wachimbaji wadogo wengi hawana uwezo wa kununua vifaa vya kisasa vya uchimbaji na hivyo kufanya kazi zao kwa kutumia vifaa duni ambavyo havna tija katika uchimbaji.
Katika kutatua changamoto ya teknolojia kwa wachimbaji wadogo, Serikali kupitia STAMICO tayari imeshanunua mitambo mitano yenye thamani ya shilingi bilioni 2.22 na imepanga kununua mitambo hiyo mengine 10 ili kufikia idadi mitambo 15 kwa ajili ya Wachimbaji Wadogo.
Mitambo ya uchorongaji imeleta maboresho makubwa kwa wachimbaji wadogo kwa njia kadhaa ikiwemo kuongeza ufanisi katika uchimbaji wa madini, ikiruhusu uchimbaji wa kina na salama zaidi kuliko mbinu za asili sambamba na kupunguza gharama na muda wa uzalishaji, kwa ujumla, mitambo ya uchorongaji imeboresha mazingira ya kazi, kuleta tija, na kuongeza kipato kwa wachimbaji wadogo.
Hatua za Serikali na Wadau Wengine Kuwawezesha Wachimbaji Wadogo
Serikali imechukua hatua mbalimbali kuwawezesha wachimbaji wadogo kukabiliana na changamoto zao.Kupitia Tume ya Madini, Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kurahisisha utoaji wa leseni na kutoa elimu juu ya uchimbaji salama na wenye tija.
Juhudi nyingine ni pamoja na ziara za mafunzo ambazo zinaratibiwa Wizara kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo Tanzania (FEMATA), kwa mfano Kwa mwaka 2023 Wachimbaji Wadogo walifanya ziara maalum ya mafunzo nchini China, ambapo walipata fursa ya kutembelea viwanda vinavyotengeneza mitambo na vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji wa madini. Katika ziara hiyo, wachimbaji hao walipata ujuzi, uzoefu, na kujifunza kuhusu teknolojia mpya.
Ustawi wa tasnia ya uchimbaji mdogo wa madini nchini Tanzania, umekuwa wa kuvutia kiasi cha baadhi ya mataifa kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara kuomba kuja kujifunza hapa nchini kuhusu usimamizi na uendeshaji wa sekta ya madini ikiwemo uchimbaji mdogo.
Mchango wa wachimbaji wadogo wa madini nchini Tanzania ni mkubwa na hauwezi kupuuzwa. Wanatoa ajira, kuongeza pato la taifa, na kuchangia maendeleo ya jamii. Serikali kupitia Wizara ya Madini na taasisi zake zinazohusika zinaendelea kuweka mazingira wezeshi na kutoa msaada unaohitajika ili wachimbaji wadogo waweze kuchangia zaidi katika maendeleo ya Sekta ya Madini na uchumi kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment