Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameshiriki Jubilei pacha ya miaka 50 ya upadre, na miaka 25 ya Uaskofu ya Askofu Mstaafu Desiderius M. Rwoma wa Jimbo Katoliki la Bukoba mkoani Kagera.
Jubilei hiyo imefanyika leo, tarehe 02 Agosti 2024 katika Kanisa Kuu Katoliki Jimbo la Bukoba ambapo imeambatana Misa ya kumpongeza Askofu Mstaafu, Method Kilaini pamoja na Mhashamu Askofu Jovitus Mwijage Kwa kuwekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba.
Katika Jubilei hiyo, Waziri Bashungwa amewasilisha Salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Maaskofu hao na waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba.
“Niwaletee salamu za Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae alitamani kuwa nasi katika siku ya leo ya kihistoria ya kufurahia na kusherekea miaka 50 ya upadre, na miaka 25 ya Uaskofu ya Askofu Mstaafu Desiderius M. Rwoma” amesema Bashungwa
Aidha, Waziri Bashungwa amelishukuru Kanisa Katoliki kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii hususani sekta ya elimu, afya na shughuli za uzalishaji.
Katika Jubilei hiyo, Waziri Bashngwa alipata nafasi ya kueleza kazi na miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya sita katika sekta ya ujenzi ambayo ni pamoja na Upanuzi kwa njia 4 barabara ya Rwamishenye hadi Stendi ya Mjini, Ujenzi wa barabara ya Karagwe – Benako, Ukarabati wa barabara ya Lusahunga- Rusumo na miradi mingine.
Bashungwa ametoa wito kwa Viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa, kumuombea Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine wote, ili mwenyezi Mungu aendelee kuwawezesha katika kazi wanayoifanya katika kutliumikia Taifa.
Kwa Upande wake, Askofu Mstaafu Mhashamu Desiderius Rwoma amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumzawadia Uaskofu, pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukubali kuwa mgeni rasmi katika Jubilei yake na kumtuma Waziri wa Ujenzi, innocent Bashungwa kumwakilisha.
No comments:
Post a Comment