BILIONI 840 KUTUMIKA UJENZI WA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIWA NA EL-NINO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 22, 2024

BILIONI 840 KUTUMIKA UJENZI WA MIUNDOMBINU ILIYOATHIRIWA NA EL-NINO

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akifafanua jambo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu wakati akiwasilisha taaarifa ya mkakati wa Serikali kuhusu Ukarabati wa Miundombinu ya Barabara iliyoharibiwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya leo tarehe 22 Agosti, 2024 Mkoani Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso (Mb), akitoa maelekezo kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (hayupo pichani), mara baada ya kupokea taaarifa ya mkakati wa Serikali kuhusu Ukarabati wa Miundombinu ya Barabara iliyoharibiwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya leo tarehe 22 Agosti, 2024 Mkoani Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, wakisikiliza taaarifa ya mkakati wa Serikali kuhusu Ukarabati wa Miundombinu ya Barabara iliyoharibiwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya kutoka kwa Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (hayupo pichani)leo tarehe 22 Agosti, 2024 Mkoani Dodoma.


Na Mwandishi Wetu, Dodoma 


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali tayari imeelekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 840 (Dola za Marekani Milioni 325) katika ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na makalvati yaliyoharibiwa na mvua kubwa za El-Nino na Kimbunga Hidaya ambapo maandalizi ya utekelezaji huo yanaendelea.

Ameeleza kuwa mvua za El-Nino zilizonyesha katika kipindi cha mwezi Septemba 2023 hadi Aprili 2024 na kuathiri mawasiliano ya barabara na madaraja, Serikali ilitoa kiasi cha Shilingi Bilioni 72.1 kufanya matengenezo ya dharura katika maeneo yaliyokatika mawasiliano.

Bashungwa ameeleza hayo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu leo Agosti 22, 2024 wakati akiwasilisha taaarifa ya mkakati wa Serikali kuhusu Ukarabati wa Miundombinu ya Barabara iliyoharibiwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya.

“Wizara imeona umuhimu wa kuanza ujenzi wa madaraja na makalvati kwa kuwa mvua inaponyesha pindi kunapokuwa na barabara mawasiliano yanaendelea kuwepo hata kama ni kwa shida lakini daraja ama kalvati linapovunjika linasababisha mawasiliano kukosekana kabisa”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameongeza kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali ili kuhakikisha kuwa miundombinu yote iliyoathiriwa inafanyiwa matengenezo ili irudi katika hali yake ya awali ambapo tathimini ilionesha kiasi cha Shilingi Trilioni 1.07 kinahitajika kwa ajili ya matengenezo ya miundombinu yote iliyoathiriwa.

Aidha, Bashungwa ameielekeza Wakala ya Barabara (TANROADS), kuhakikisha inafanya mapitio mapya ya barabara zilizofanyiwa usanifu miaka ya nyuma ili kuweza kutekeleza ujenzi na matengenezo kulingana na uhalisia, Mabadiliko ya Mazingira, Ongezeko la watu na ukuaji wa Miji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Selemani Kakoso (Mb), ameishauri Wizara ya Ujenzi kushirikisha Waheshimiwa Wabunge katika maeneo yaliyolengwa ili utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya barabara na madaraja iliyoathiriwa ufanyike kwa tija na mahitaji halisi ya maeneo husika.

Kakoso ameitaka Wizara ya Ujenzi kuusimamia kikamilifu Wakala wa Barabara (TANROADS) na Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) kuhusu upatikanaji wa vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza wigo mpana wa kupata fedha kwa ajili ya mipango ya baadae ya ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi

No comments:

Post a Comment