Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza wakati akifungua Mkutano wa kuwajengea uwezo Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya, kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma na Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na Matumizi Sahihi ya Takwimu, tukio lililofanyika ukumbi wa Jiji, uliopo mji wa Magufuli-Mtumba, jijini Dodoma, ambapo amewasihi viongozi hao kutumia vyema mafunzo hayo katika kutekeleza majukumu mbalimbali katika ununuzi wa vifaa na utekelezaji wa miradi kupitia Mfumo wa Ununuzi wa umma (Nest) na fursa ya kutekeleza miradi kwa njia ya Ubia.
Na Okuly Julius , DODOMA
Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amezitaka Mamlaka za serikali pamoja na wawekezeji kutoka sekta binafsi kutumia fursa zilizopo katika sheria ya PPP kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo ili kuipunguzia serikali mzigo wa kibajeti.
Dkt. Nchemba ameyasema hayo leo Agosti 31 ,2024 jijini Dodoma katika Mkutano wa mafunzo ya Sheria ya Ununuzi wa Umma na Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi na Matumizi sahihi ya Takwimu kwa Wakuu wa Mikoa ,Makatibu Tawala wa Mikoa ,Wakuu wa Wilaya ,Wakurugenzi wa Halmashauri,Waganga wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya.
Pia Dkt. Nchemba amewaagiza Maafisa Masuuli wote nchini kuzingatia maelekezo ya waraka wa Hazina namba 7 wa mwaka 2020 -2021 unaotoa maelezo na muongozo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa utaratibu wa PPP
“Taifa lolote ulimwenguni lina matumizi sahihi ya Takwimu zilizozalishwa na vyombo vyenye jukumu hilo kwa mnaofahamu maendeleo yeyote ya nchi yatafanyika kwa mafanikio endapo Takwimu sahihi zitatumika,” amesema
Hata hivyo Dkt.Nchemba amesema eneo muhimu lililowekwa katika sheria ya ununuzi wa umma kwa makusudi ya kuwainua watanzania ni ushiriki wa kampuni za Kitanzania katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, ambapo katika hilo kampuni za kitanzanaia ndizo zitakazopaswa kuwa kampuni kiongozi ambazo ndizo zitakazokuwa na jukumu la kutafuta kampuni nyingine itakayoshirikiana nazo katika utekelezaji wa mradi husika ,ikiwemo kusimamia thamani ya fedha.
Aidha ametoa wito kwa watanzania kujenga tabia ya kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili kuendelea kukuza uchumi wa ndani ya nchi.
“Kumekuwa na wimbi la watanzania kuamini kuwa bidhaa kutoka nje ndio imara na kuacha kutumia bidhaa za ndani yaani unakuta mtanzania anakwenda kufungua kiwanda nje ya nchi ili aingize tu bidhaa kutoka nje wakati anaweza kufungua kiwanda hicho ndani ya nchi na kuzalisha hapahapa nchini ili kujenga uchumi wa ndani,” ameeleza Nchemba
Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt . Festo Dugange ameelezea changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza kutumia mfumo mpya wa manunuzi wa (NeST) hasa katika utekelezaji wa miradi inayotumia FORCE ACCOUNT.
Ambapo amesema kutokana na Mfumo huo umesababisha kasi kupungua ila katika mafunzo hayo anaamini kuwa elimu itakayotolewa itasaidia kutoa jibu sahihi ili kusaidia utekelezaji wa miradi bila kusuasua.
Serikali imetunga na kupitisha Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 10 ya Mwaka 2023 na kuifuta Sheria ya Ununuzi wa Umma Na. 7 ya mwaka 2011 (pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2016) na kusisitiza misingi ya kuwepo kwa usawa, kupatikana kwa thamani halisi ya fedha, uwazi, ushindani wa haki pamoja na uwajibikaji. Sheria mpya ya Ununuzi imejikita zaidi katika kulinda maslahi ya Taifa hususan katika kuwanufaisha watanzania.
No comments:
Post a Comment