Dkt. Tulia Ahamasisha Wananchi Kutoa Maoni, Dira 2050 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, August 4, 2024

Dkt. Tulia Ahamasisha Wananchi Kutoa Maoni, Dira 2050



Na Adelina Johnbosco, Mbeya.


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb), ametoa wito kwa Watanzania kutoa maoni kwa ajili ya kupata Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa manufaa yao wenyewe na taifa bila kujali nafasi ama vyeo walivyo navyo katika jamii

Ametoa rai hiyo wakati akihutubia wananchi jijini Mbeya kwenye uzinduzi wa kongamano la wadau na wananchi wa Nyanda za Juu Kusini, kuhusu ukusanyaji wa maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika Ukumbi wa Mikutano wa Eden Highlands Hotel, leo Agosti 3, 2024, ambapo alikuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo.

"Ugeni rasmi kwenye uzinduzi huu nitauacha hapa, baada ya kutoka hapa nami nitashiriki kutoa maoni yangu kama mwananchi na nitahamasisha wananchi kutoa maoni yao bila kujali nafasi zao walizonazo katika jamii, kinachohitajika ni maoni,” Dkt. Tulia amesisitiza.

Vile vile, amebainisha juu ya urithishwaji wa maisha mazuri kutoka kwa wazazi waliopo leo kwenda kizazi kijacho, kuwa yatategemea maoni yenye tija kutoka kwa wazazi waliopo leo.

Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, ametoa rai kwa viongozi wote nchini kuwa na nia moja ya kujikita kwenye kuwapeleka wananchi sehemu moja ya maendeleo waliyoichagua kwenye Dira na si vinginevyo.

"Zinaweza kutumika njia tofauti za kuwaongoza wananchi, lakini lengo liwe moja na jema la kuwaweka wananchi kwenye maendeleo kutokana na maoni yao, ili kukidhi maslahi yao na taifa kwa ujumla," amesema Prof. Mkumbo.

Akiongea kwa niaba ya wakuu wa mikoa inayounda Nyanda za Juu Kusini ambayo ni Iringa, Njombe, Mbeya na Songwe, Mkuu wa mkoa Iringa, Mhe. Peter Serukamba, amewataka wananchi wa nyanda hizo kuchangia maoni, ili nchi iweze kupanga mipango inayoendana na mahitaji yao husika.

"Nyanda za Juu Kusini ni miongoni mwa mikoa hapa Tanzania inayolisha nchi, mikoa yetu inalima mazao ya chakula kwa wingi, inaifanya nchi kuwa na utoshelevu wa chakula. Tutoe maoni ili Serikali ijue ni vipi izidi kutuendeleza katika nyanja mbalimbali hasa kwenye kilimo" amesisitiza Mhe. Serukamba

Sambamba na hayo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Thobias Makoba, ameongoza mjadala wa utoaji maoni kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa wananchi waliohudhuria kongamano hilo ikiwa ni sehemu ya ukusanyaji wa maoni ya wananchi.

No comments:

Post a Comment