Na MwandishiWetu, Dodoma
Maonesho ya Wakulima(Nanenane)yakiwa yanaendelea Jijini hapa, Baraza la Ushauri la watumiaji wa huduma za Nishati na Maji (EWURA CCC) limeendelea kutimiza wajibu wake kwa kuwaelimisha wananchi namna ya matumizi sahihi ya gesi.
Hatua hii itawasaidia Wananchi kufahamu jinsi ya kutumia gesi kwa usalama ikiwa ni pamoja na kuelewa jinsi ya kuunganishwa kwa usahihi, kutambua dalili za uvujaji, na jinsi ya kutengeneza tatizo la gesi ikiwa linatokea.
Afisa Msaidizi huduma kwa Wateja na Utawala Dodoma(COMA)Amani Mbogo ameeleza kuwa Elimu kuhusu jinsi ya kubaini uvujaji wa gesi ni muhimu ambapo wananchi wanapaswa kujua alama za uvujaji kama harufu ya gesi au kutumia vifaa vya kupima uvujaji kama vile mashine za gesi.
Akizungumza na Gazeti la Majira Agosti 7,2024 kwenye maonesho hayo yanayoendelea kwenye viwanja Nzuguni Dodoma Mbogo amesema Wananchi wanahitaji kuelewa umuhimu wa kutunza vifaa vya gesi kama vile mitungi na vichoma moto.
"Hii inajumuisha kufuata ratiba ya ukaguzi na matengenezo ili kuhakikisha vifaa vinaendelea kuwa salama, " amesisitiza
Kuhusu hatari za Gesi,Afisa huyo ameeleza kuwa Elimu kuhusu hatari zinazohusiana na gesi, kama vile sumu au moto, ni muhimu na kwamba Wananchi wanapaswa kuchukua hatua za dharura, kama vile kuondoka kwenye eneo lililoathirika na kuwasiliana na huduma za dharura.
"Ni wajibu wetu EWURA CCC kuwaelimisha wananchi ,Wananchi wanapaswa kufahamu mikakati ya kujilinda, ikiwa ni pamoja na kuwa na mipango ya dharura ya familia na kuhakikisha kuwa nyumba zao zina vifaa vya kudhibiti moto ili kuwa salama, " ameleeza Mbogo
Pamoja na hayo ameeleza Sheria na kanuni zinazohusiana na matumizi ya gesi kuwa inasaidia wananchi kutekeleza taratibu zinazotakiwa na kuepuka matatizo ya kisheria ikiwa ni pamoja na kufahamu jinsi ya kupata msaada kutoka kwa watoa huduma wa gesi na mamlaka zinazohusika endapo watakumbana na matatizo au maswali kuhusu matumizi ya gesi.
"Baraza hili lina jukumu la kuwakumbusha watumiaji wa gesi ya kupikia majumbani kuwa na wajibu wa kutunza mazingira, aidha wasambazaji wa gesi wanatakiwa kuchukua tahadhari ili kuongeza usalama wa afya za watumiaji na mali zao kama inavyoelekezwa kwenye kanuni ya 22(1) ikiwaelekeza wasambazaji wakubwa na wadogo wachukue tahadhari, "amefafanua.
No comments:
Post a Comment