Kamati ya Bajeti kutoka Baraza la Wawakilishi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekamilisha ziara yake mkoani Arusha na kutoa pongezi kwa Wizara ya Maji kwa kukamilisha mradi mkubwa wa Uboreshaji wa Huduma ya Maji jijini Arusha.
Ziara hiyo ya siku mbili imetumika kutembelea mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 520 ambapo kamati imejionea miundombinu ya mradi inayohusisha mabwawa makubwa ya kutibu majitaka, visima vilivyochimbwa sehemu mbalimbali ndani na nje ya jiji la Arusha na matenki makubwa ambayo yamewezesha sehemu kubwa ya jiji la Arusha na maeneo jirani kupata huduma majisafi, salama na yenye kutosheleza.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Mwanaasha Hamis amesema hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa mradi huo ni kubwa na kwamba Zanzibar inalo la kujifunza hasa suala zima la utunzaji wa vyanzo vya maji. Amesema mradi huo ni mkubwa na wa kisasa . Pia unahitaji maji mengi kwa ajili ya jiji la Arusha ambalo ni moja ya majiji ya utalii hapa nchini. Zanzibar pia ni maarufu kwa utalii hivyo inapaswa kujifunza namna Arusha wanavyosimamia na kuendeleza utunzaji wa mazingira ili miradi ya maji iwe endelevu.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jiji la Arusha Mhandisi Justine Rujomba amesema wafanyakazi wa Mamlaka ya Majisafi Arusha wanayo mengi ya kujifunza kutoka Zanzibar. Amesema mradi huo umehakikisha unajali mazingira kwa kujenga mabwawa ya kutibu majitaka ambayo yanaweza kuhudumia jiji la Arusha kwa miaka ishirini ijayo. Ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa jiji la Arusha kujitokeza kuunganisha majitaka katika miundombinu hiyo.
Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wizara ya Maji Mteki Chisute ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ubora wa Maji Wizara ya Maji Tanzania Bara amesema malengo ya viongozi wa pande mbili za muungano ni kuhakikisha huduma ya majisafi na salama inafikishwa kwa kila Mtanzania hivyo Wizara ya Maji itahakikisha ushirikiano huo unadumu.
No comments:
Post a Comment