Takribani watu 12 sasa wameripotiwa kufariki dunia baada ya kutokea maporomoko ya udongo katika eneo kubwa la kutupa taka katika mji mkuu wa Uganda, Kampala.
Waokoaji wanaendelea kuchimba uchafu huo kwa matumaini ya kupata manusura zaidi baada ya maporomoko hayo yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha kwa wiki kadhaa.
Jalala la Kiteezi lenye ukubwa wa ekari 36 (hekta 14) ndilo pekee linalohudumia Kampala nzima, jiji ambalo linakadiriwa kuwa na watu milioni nne.
Mamlaka za jiji zimeripotiwa kujaribu kutafuta eneo jipya kwa miaka mingi.
Kilima kikubwa kilichoundwa na mrundikano wa takataka kiliporomoka Ijumaa usiku, na kufunika nyumba kwenye ukingo wa eneo hilo wakati wakazi walikuwa wamelala, linaripoti shirika la habari la Reuters.
Siku ya Jumamosi, idadi ya waliofariki ilitolewa kuwa wanane, wakiwemo watoto wawili.
Msemaji wa polisi wa Kampala Patrick Onyango aliambia AFP siku ya Jumapili kwamba miili minne zaidi imetolewa, huku watu 14 wakiokolewa.
No comments:
Post a Comment