Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 22 Agosti, 2024
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu ameitaka Tume ya Utumishi wa Umma kupokea na kushughulikia changamoto za watumishi wa umma kwa wakati ili kujenga imani kwa watumishi kupitia taasisi hiyo na kupata suluhisho la changamoto hizo kwa muda sahihi.
Naibu Waziri Sangu, ameyazungumza hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika ofisi hiyo iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi ambapo amewatala kuwa wazalendo katika kutekeleza majukumu yao.
Aidha Mhe. Sangu ameitaka menejimenti hiyo kuongeza mawanda na kuwa na ubunifu katika kutoa huduma kwa watumishi ili kutoa uhuru wa kujieleza pale ambapo watumishi watahitaji kuwasiilisha changamoto au malalamiko mbalimbali.
Awali akitoa neno la utangulizi, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew Kirama amesema kuwa waajiri katika mamlaka za ajira na mamlaka za nidhamu wanatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia Sheria, Taratibu, Kanuni na Miongozo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Idara ya Rufaa na Malalamiko, Bw. John Mbisso akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri Sangu amesema kuwa, menejimenti imepokea maelekezo yote na kuahidi kuyafanyia kazi kwa ukamilifu.
No comments:
Post a Comment