Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Ruvuma.
Licha ya Jiografia ya Wilaya ya Madaba kuwa na maeneo yenye milima na mabonde yanayosababisha maeneo ya bondeni kukosa huduma za mawasiliano, Serikali imeahidi kuhakikisha wilaya hiyo yote inapata huduma bora za mawasiliano ili wananchi wake washiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.
Ahadi hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) wakati akizungumza na Wanakijiji cha Maweso akiwa katika ziara ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika vijiji tisa vya wilaya ya Madaba mkoani Ruvuma tarehe 16 Agosti 2024.
Akiwa wilayani Madaba ametembelea vijiji vya Igawisenga, Wino, Maweso, Mwande, Matetereka, Mkongotema, Lutukira, Ndelenyuma, Gumbiro na Mbangamawe ikiwa ni pamoja na kuzungumza na wananchi na kupata mrejesho wa hali ya huduma za habari na mawasiliano katika vijiji hivyo.
“Tunatambua Jiografia ya Wilaya yenu ni ya milima na mabonde, lakini Serikali itahakikisha Madaba yote inapata huduma bora za mawasiliano ili mshiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali”, amesisitiza Mhandisi Mahundi.
Mhandisi Mahundi ametaja jitihada ambazo Serikali inaendelea kufanya ili kuboresha huduma za mawasiliano katika wilaya ya Madaba kuwa ni pamoja na ujenzi wa minara mipya ya mawasiliano.
Ametaja jitihada nyingine kuwa ni kuboresha teknolojia ya minara iliyopo, na kuongeza vifaa kwenye kituo cha Mkongo wa Taifa cha Madaba ili kukiongezea nguvu ya kuwezesha huduma za uhakika za mawasiliano.
Naye Bw. Philemon Machaine, akimwakilisha Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara hiyo amesema Serikali kwa kushirikiana na watoa huduma itaendelea kuboresha huduma za mawasiliano, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watoa huduma wanaweka nishati ya umeme kwenye miradi ya mawasiliano inayotumia nishati ya jua ili mawasiliano yawe ya uhakika.
Katika ziara hiyo, Mhandisi Mahundi pia aliambatana na Mhandisi Shirikisho Mpunji kutoka Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Bw. Zablon Magabula, Mwakilishi wa Meneja wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) mkoa wa Ruvuma.
Katika hatua nyingine Mhandisi Mahundi alitumia fursa hiyo kuwahamasisha wananchi kushiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba 2024, na kutoa rai kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi huku akiwataka wanaume kuwaunga mkono wanawake watakaojitokeza kugombea.
No comments:
Post a Comment