Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Philip Mpango amewapongeza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), na kuwataka waendelee kusimamia barabara.
Dkt Mpango ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Agosti, 2024 kwenye banda la maonesho ya Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani la Wizara ya Ujenzi na taasisi zake yanayofanyika jijini Dodoma kwenye uwanja wa Jamhuri.
Dkt. Mpango pia amewataka TANROADS kuhakikisha kila mradi wa ujenzi wa barabara unakuwa na njia za waenda kwa miguu, baiskeli na pikipiki ili kuwakinga na ajali za kugongwa na magari.
“Katika barabara zetu tuweke sehemu za watembea kwa miguu, pikipiki na hata baiskeli ili kuwalinda na ajali za magari,” amesisitiza Dkt. Mpango.
Halikadhalika, alitaka kufahamu namna TANROADS inavyowadhibiti madereva wenye magari makubwa yanayobeba mizigo wanaokwepa kupita kwenye mzani kwa ajili ya kupimwa mizigo, ambapo mmoja wa Wataalam Mhandisi George Daffa amesema wanadhibiti kwa kuwakamata mara wanapoonekana kwenye kamera za ufutiliaji wa matukio (CCTV) zilizofungwa kwenye vituo 13 hadi sasa.
Awali katika ufunguzi wa maadhimisho hayo, Dkt Mpango amelitaka Baraza la Taifa la Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kuhakikisha wanasimamia ukaguzi wa vyombo vya moto mwaka mzima na sio kusubiri kipindi cha wiki ya Nenda kwa Usalama pekee.
Maadhimisho hayo ya miaka 50 ya Baraza hilo yamebebwa na kaulimbiu ya ''Endesha Salama, Ufike Salama"
No comments:
Post a Comment