TANZANIA YAJIVUNIA MAENDELEO YA KIDIJITALI KUPITIA MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 27, 2024

TANZANIA YAJIVUNIA MAENDELEO YA KIDIJITALI KUPITIA MRADI WA TANZANIA YA KIDIJITALI



Na Mwandishi Wetu, Arusha.




Tanzania inajivunia hatua ilizochukua za kuziba pengo la kidijitali nchini kwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za mtandao wa kasi kwa taasisi za Serikali na kwa umma kwa ujumla kupitia utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.


Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla ameyasema hayo leo Agosti 27, 2024 akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mradi huo kinachofanyika kwa wiki nzima jijini Arusha.


Aidha, amesema kuwa anatambua mchango mkubwa wa Benki ya Dunia wa kuwezesha mapinduzi ya uchumi wa kidijitali nchini kupitia ufadhili wa mradi wa Tanzania ya kidijitali ambao pamoja na mambo mengine unahakikisha jamii zote za watanzania haziachwi nyuma katika zama hizi za kidijitali.




“Kupitia mradi huu hatujengi tu miundombinu bali tunatengeneza fursa za kidijitali kwa watanzania kwa kuwaunganisha na huduma za kidijitali na kuweka msingi imara wa bunifu za TEHAMA zitakazolipeleka taifa letu mbele.”, amezungumza Katibu Mkuu Abdulla.


Bwana Abdulla amesema lengo la Serikali kupitia Wizara hiyo ni kukuza uchumi wa kidijitali kwa kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa chini ya mradi wa Tanzania ya kidijitali inafanyika kwa ubora na kasi inayotakiwa ili kuijenga Tanzania yenye uwezo mkubwa wa matumizi ya teknolojia ya kidijitali.


Ameizungumzia miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa minara 758 Tanzania Bara na Zanzibar, itakayowezesha mawasiliano vijijini na kuwezesha upatikanaji wa huduma ya mtandao wa kasi kwa ofisi 968 za umma ili kuongeza uwajibikaji na ufanisi.

Eneo jingine alilolizungumzia ni kuwajengea uwezo wataalamu wa TEHAMA 500 kwa kufadhili mafunzo ya muda mrefu na mfupi ndani na nje ya nchi ambapo mpaka sasa watumishi wa umma 50 tayari wanaendelea na mafunzo ya muda mrefu nje ya nchi maeneo ya teknolojia zinazoibukia.

Kwa upande wake Bw. Paul Seaden, Kiongozi wa Kikosi kazi kutoka Benki ya Dunia amesema kuwa kikao hicho cha tathmini ya mradi ni muhimu ili kufanya mapitio na kuhakikisha mradi unaendelea kutekelezwa kwa ufanisi na matokeo chanya.

Aidha, ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano mkubwa inayoutoa na wapo tayari kumalizia miaka miwili iliyobakia ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa Tanzania ya Kidijitali.

No comments:

Post a Comment