"WANAWAKE TUMIENI FURSA KUSHIRIKI CHAGUZI KUFIKIA USAWA WA KIJINSIA" RC SENYAMULE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, August 28, 2024

"WANAWAKE TUMIENI FURSA KUSHIRIKI CHAGUZI KUFIKIA USAWA WA KIJINSIA" RC SENYAMULE


Wanawake wa Kata ya Haubi, Wilaya ya Kondoa, wameshauriwa kutumia fursa zilizowekwa na Serikali ili kufikia usawa wa jinsia. Hayo yamebainishwa Agosti 27, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary S. Senyamule alipokua anafungua Tamasha la Saba la jinsia ngazi ya Wilaya 2024 linalofanyika katika viwanja vya sabasaba Wilayani humo kwa siku tatu.

Mkuu huyo wa Mkoa, amezitaja fursa mbalimbali lakini kubwa zaidi ni kuwasisitiza Wanawake wenye sifa za kugombea uongozi kufanya hivyo kwa kushiriki chaguzi mbalimbali.

"Tutumie nafasi hii kusema tunataka nini katika kufikia usawa wa kijinsia ifikapo 2050. Hapa tumepewa nafasi kwani nasikia kuna banda kwa ajili ya wananchi kutoa maoni yenu, tuitumie fursa hii adhimu. Wanawake, tushiriki kwenye chaguzi kwani tayari Mhe. Rais ametuonesha ari yake" Amesema Mhe. Senyamule.

Aidha, Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Mhe. Fatma Nyangasa, amesema Serikali ya Wilaya imepiga hatua katika kusimamia masuala ya jinsia kwa kuimarisha afua zake pamoja na kuhakikisha huduma za maji, nishati Safi na mikopo kwa Wanawake inapatikana huku mpango wa utambuzi, ufuatiliaji na utatuzi wa changamoto zinazowakabili Wanawake zikiendelea.

Kadhalika, Mkurungenzi Mtendaji wa TGNP Bi. Lilian Liundi, amesema Taasisi yake ilianzisha mitandao ya jinsia ngazi za Wilaya ili kuwawezesha harakati zenye mrengo wa kijinsia na maendeleo kufika katika ngazi hiyo na kumkomboa mwanamke.

Tamasha la Saba la jinsia ngazi za Wilaya 2024, limeandaliwa mahsusi kwa siku tatu likiwa na lengo la kuangazia masuala ya haki za Wanawake na jinsia kwa ujumla. Tamasha la kwanza Kitaifa lilianza mwaka 1996 na kufanikiwa kuwafikia watu zaidi ya Milioni 15. Dhima ya Tamasha la mwaka huu ni "Dira ya maendeleo jumuishi 2050: miaka 30+ ya Beijing, tujipange"



No comments:

Post a Comment