Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe Dkt. Doto Biteko ameliitaka Shirika la Umeme Tanzania ( TANESCO) kutumia fursa ya uwepo wa umeme wa kutosha katika kipindi hiki kufanya matengenezo ya mashine mbalimbali ambazo hazikuweza kufanyiwa matengenezo kipindi ambacho nchi ilikuwa haina umeme wa kutosha.
Dkt Biteko ameyasema hayo leo 11 Agosti, 2024 jijini Dar es Salaam wakati alipofanya ziara ya kutembelea vituo vya umeme vya Ubungo I, Ubungo II, Ubungo III pamoja na kituo cha kudhiti mifumo ya umeme wa gridi yaani Grid control Centre.
Dkt. Biteko ameitaka TANESCO kuhakikisha matengenezo ya miundombinu ya umeme yanakuwa endelevu ili watanzania wapate umeme wa uhakika.
‘’Kwakweli namshukuru Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa msukumo wake mkubwa katika Sekta ya Nishati na sisi kama Wizara kupitia Tanesco tutaendelea kuhakikisha watanzania wanapata umeme wa uhakika.’’ Amesema Dkt. Biteko
Amesema kwa sasa kuna ziada ya umeme na ndio maana matengenezo yanaweza kufanyika kwenye mitambo katika vituo vya Kidatu, Kihansi na Mtera na hivi karibuni TANESCO itakamilisha matengenezo kwenye laini za Mikoa ya Kaskazini ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme ambapo amewashukuru wananchi wa mikoa hiyo kwa uvumilivu wao katika kipindi chote cha matengenezo.
Amesisitiza kuwa, kwa sasa hali ya upatikanaji wa umeme ni ya kuridhisha hasa ikizingatiwa kuwa mradi wa bwawa la kufua umeme la Julius Nyerere unaendelea vizuri na tayari mashine tatu zimeshaungwa kwenye gridi ya Taifa na mashine ya nne inatarajiwa kuingizwa mwezi huu na kwamba tayari mashine tatu za mradi wa Rusumo zinafanya kazi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti Mifumo, Mha. Deogratius Mariwa amesema kwa sasa TANESCO inafanya maboresho kwenye mfumo wake wa Gridi ili uende sambamba na mahitaji ya sasa kwa kujenga vituo 5 vya kanda vya kudhibiti mifumo ya gridi sambamba na vituo vya ziada vitakavyosaidia wakati wa hitilafu za umeme.
Amesema mipango iliyopo kwa sasa ni kuongeza vituo takribani 20 katika kipindi cha miaka 3 sambamba na kuunganisha mifumo ya gridi na nchi za Kenya, Uganda, Zambia na baadaye Msumbiji ili kuinarisha mifumo ya upatikanaji umeme.
Amesema Vituo hivyo vitajengwa kwenye mikoa ya Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Mbeya, na Dodoma ambapo kwa sasa wako kwenye hatua za kumpata mkandarasi na kuongeza kuwa kwa sasa kuna jumla ya vituo 67 vya gridi.
Ziara hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio pamoja na Menejimenti ya TANESCO.
No comments:
Post a Comment