Adelina Johnbosco, Zanzibar
Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amewataka Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika zoezi la kutoa maoni yatakayowezesha kuandaliwa kwa Dira ya Taifa 2050.
Ametoa rai hiyo leo Agosti 28, 2024, ofisini kwake mjini Magharibi wakati akiongea na wajumbe wa Tume ya Mipango na Timu Kuu ya Wataalamu ya Dira ya Taifa 2050 iliyoongozwa na mjumbe wa Tume ya Mipango na Mwenyekiti wa Timu hiyo, Dkt. Asha Rose Migiro.
"Watanzania wote waendelee kutoa maoni yao ili tuweze kupata Dira tunayoitaka, asitokee mtu tukishapata Dira akasema sikupata fursa ya kutoa maoni, makundi yote waone umuhimu wa kushiriki kutoa maoni, hili ni jambo muhimu na lenye manufaa katika kuisaidia nchi yetu," alisisitiza Mhe. Abdulla
Vilevile, amehimiza ulazima wa kila Mtanzania kuhakikisha anadumisha amani na utulivu ili mipango ya maendeleo ya Dira 2050 iweze kutekelezwa kikamilifu.
Katika hatua nyingine, Mhe. Abdulla, amewakaribisha Wananchi wote katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), siku ya Jumamosi Agosti 31, 2024, ili kushiriki katika kongamano la kutoa maoni kwa ajili ya Dira ya Taifa 2050 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla.
No comments:
Post a Comment