BoT, AZAKI WAJADILI KUBORESHA HUDUMA JUMUISHI ZA FEDHA KWA JAMII - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 13, 2024

BoT, AZAKI WAJADILI KUBORESHA HUDUMA JUMUISHI ZA FEDHA KWA JAMII


Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Fedha, Idara ya Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dastan Massawe, Akizungumza katika mdahalo wa kujadili Biashara Jumuishi kati ya Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia uliofanyika Septemba 12, 2024 Jijini Arusha.

Mkuu wa Programu kutoka Shirika la Foundation For Civil Society (FCS) Nasim Losai,akizungumza alipokuwa akitoa maelezo ya awali kuhusu mdahalo huo.



Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA - CCC) Mary Msuya, (kulia), akizungumza namna taasisi yao inavyotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

PICHA NA; FCS Na; Hughes Dugilo, ARUSHA

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema itaendelea kufanya jitihada mbalimbali za kusaidia ukuaji wa huduma za malipo kidigitali kwa kuweka miundombinu rafiki ili kuhakikisha inamlinda mwananchi katika shughuli za uchumi ikiwemo kuwa na unafuu wa kutuma miamala ya fedha.

Akizungumza Jijini Arusha katika mdahalo wa kujadili Biashara Jumuishi kati ya Sekta Binafsi na Asasi za Kiraia, Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Fedha, Idara ya Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dastan Massawe, amesema kuwa Benki hiyo inatambua umuhimu wa huduma za fedha kama chachu ya ukuaji wa biashara na uchumi nchini.

Massawe amesema BoT inaendelea na jitihada za kuwezesha biashara ya ndani na nje ya nchi pamoja na kuangalia usalama wa fedha ili kuondokana na changamoto zinazojitokeza ikiwemo uwepo wa matapeli mtandaoni.

Amesema kuna sera wezeshi ambazo haziingiliani na sera nyingine zenye ubunifu katika mifumo inayoimarisha usalama wa miamala baina ya wafanyabiashara mbalimbali.

“Wafanyabiashara wengi bado hawajafikiwa na huduma rasmi za kifedha, asilimia kubwa wanafanya biashara nje ya mifumo, hivyo kuwakosesha fursa ya kupata mitaji” Amesema Massawe.

Kwa upande wake Mkuu wa Programu kutoka Shirika la Foundation For Civil Society (FCS) Nasim Losai, amesema kuwa Shirika hilo linatekeleza mradi wa miaka mitatu wenye lengo la kuyawezesha makundi matatu ambayo ni wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwajengea uelewa mpana wa kuzitambua haki zao za msingi za masuala ya biashara na fedha.

"Kuna fursa na faida nyingi ambazo watu wanazipata lakini sio makundi yote ambayo wanaweza kupata, ndiomaana FCS tumekuja na mradi huu ili kuyafika makundi yote” Amesema Lasai.

Akizungumza katika mdahalo huo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA - CCC) Mary Msuya, amesema kuwa matumizi ya teknolojia yamerahisisha huduma jumuishi za fedha kupitia miamala ya simu tofauti na ilivyokuwa awali.

Msuya amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Juni 2024 zinaonesha kuna laini za simu milioni 76.6 zinazotumika, ambapo akaunti za fedha kwa njia ya ni simu milioni 55.7, huku watumiaji wa huduma ya internet wakiwa milioni 39.3.

Amesisitiza kuzingatia umuhimu wa kutoa na kulinda taarifa binafsi kwa watoa huduma za fedha wakati wa kujisajili, kwani baadhi yao wamekuwa sio waaminifu katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Naye mwakilishi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Perodius Makubi, amesema licha ya faida zinazopatikana katika biashara za mtandaoni kuna madhara ambayo yanajitokeza ikiwemo baadhi wa watu kwenda kinyume na malengo yaliyokusudiwa na kuleta usumbufu kwa wengine.

No comments:

Post a Comment