DARAJA LA MINYUGHE LAWAUNGANISHA WANANCHI IKUNGI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 28, 2024

DARAJA LA MINYUGHE LAWAUNGANISHA WANANCHI IKUNGI


Ikungi, Singida


Wananchi katika Wilaya ya Ikungi mkoani Singida wameeleza kufurahishwa na ukamilikaji wa Daraja la Minyughe lenye urefu wa mita 30 lililojengwa na Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).

Wakieleza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wameipongeza Serikali kupitia TARURA kwa kukamilisha mradi huo ambao umewezesha kuunganisha Kata za Minyughe na Makilawa ambapo imewezesha wananchi kuzifikia huduma za kijamii kiurahisi.

Naye, Diwani wa Kata ya Minyughe, Mhe. Nelson Kiwesi amesema kuwa hapo awali shughuli za kilimo na biashara kwa ujumla zilikwama hasa kipindi cha masika kutokana na kukosekana kwa daraja hilo.

"Tunamshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan kwa mradi huu maana ilikua vigumu kwa wananchi kuvuka upande wa pili hasa kipindi cha masika", amesema Mhe. Nelson.

Aidha, ameongeza kuwa ilikua vigumu hata kwa wanafunzi kupita eneo hilo lakini kwa sasa panapitika kwa urahisi na wanafunzi wanafika shuleni kwa wakati.

Kwa upande wake, Meneja wa TARURA Wilaya ya Ikungi, Mhandisi Ally Mimbi amesema kuwa Kata hizo zinashughuli mbalimbali za kilimo na biashara ambapo zilikwama kutokana na kutokuwepo na Daraja.

"Maeneo haya pia kuna shughuli za mnada ambazo zililazimika kusimama kabla ya kukamilisha daraja hili lakini kwasasa wananchi wanapita kwa urahisi", amesema Mhandisi Ally.

Aidha ameongeza kuwa tayari wapo kwenye mpango wa kuongeza miundombinu ya kulinda daraja hilo ili liweze kutoa huduma kwa kipindi kilichokusudiwa.

No comments:

Post a Comment