🎈🎈Mshindi wa Kwanza anyakua kitita cha milioni 5
🎈🎈 Simba, Yanga Wateka Vijana wenye Vipaji
Mashindano ya KNK CUP 2024 yaliyoandaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Mhe .Dkt. Doto Biteko ambapo timu 246 kutoka Kata 17 za Wilaya ya Bukombe imehitishwa kwa kishindo na timu ya Chui FC kutoka Kata ya Butinzya iliibuka kidedea dhidi ya timu Nyuki FC ya Kata ya Bugerenga.
Mashindano hayo yamehitimishwa katika Uwanja wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe - Kilimahewa Septemba 17, 2024, mkoani Geita na kushuhudiwa na mamia ya wananchi na viongozi ambapo Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa alikuwa mgeni rasmi.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema mshindi wa ligi ya KNK Cup ya Bukombe na mshindi wa ligi ya Bashungwa Karagwe Cup watakuwa na mechi ya kirafiki ambayo itawaunganisha vijana na kukuza vipaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za za Mitaa kwa kuchagua viongozi bora na wenye uwezo wa kuwahudumia Wananchi.
Akizungumza na wananchi walioshuhudia fainali hiyo, Waziri Bashungwa amempongeza Dkt. Biteko kuendelea kuunga mkono kwa kasi jitihada za Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye sekta ya michezo nchini kupitia ligi ambayo inaibua na kukuza vipaji na kuimarisha afya.
“Mhe. Naibu Waziri Mkuu nikupongeze kwa kazi nzuri unayoendelea kuifanya, hii ni mara ya pili unanipa heshima hii, nilipokuja hapa mwaka 2021 ligi ilikuwa imefana lakini hii ya mwaka 2024 hakika imeboreshwa kwa kiwango kikubwa”, amesema Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 15 kwa ajili ya kuboresha Uwanja wa Kilimahewa wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe ambao unatarajiwa kuwekwa nyasi na kusaidia kuongeza mapato ya Halmshauri.
Kuhusu suala la miundombinu ya barabara, Bashungwa amemuhakikishia Naibu Waziri Mkuu kuwa, Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS), tayari imeanza manunuzi ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Ushirombo – Katoro (km 59) kwa kiwango cha lami na kusisitiza hadi kufika mwishoni mwa mwezi Disemba 2024 kazi za ujenzi zitakuwa zimeanza.
No comments:
Post a Comment