Katika hafla hiyo, Bw. Mweli alisisitiza kuwa serikali imejipanga vizuri katika kumsaidia mkulima, akigusia jinsi Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeboresha bajeti ya kilimo na kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima kupata teknolojia na masoko ya mazao yao.
Maonesho hayo yalijumuisha wadau mbalimbali kutoka katika minyororo ya thamani ya mazao ya horticulture na nafaka. Wakulima walipata fursa ya kujionea teknolojia za uvunaji, uhifadhi, usindikaji, uongezaji thamani wa mazao, na vifungashio vya kisasa, vyote vikilenga kuboresha ubora na kuongeza thamani ya mazao yao.
Wadau wa sekta hiyo walihamasishwa kuchangia mawazo na teknolojia zinazoweza kusaidia katika maendeleo ya kilimo endelevu, huku wakijadili mbinu bora za kuvutia masoko na kuongeza mapato yao. Maonesho haya yanatarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Mtendaji Mkuu wa TAHA, Dkt. Jacqueline Mkindi, amemshukuru Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, pamoja na serikali kwa kuendelea kusaidia upatikanaji wa teknolojia za uhifadhi na uongezaji thamani ya mazao ya kilimo. Dkt. Mkindi alisema ushirikiano huu ni muhimu katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini na kuboresha maisha ya wakulima.
Akiwa katika maonesho, Dkt. Mkindi aliahidi kwamba TAHA itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu na serikali ili kuhakikisha malengo ya kuboresha uzalishaji na masoko yanafikiwa.
Alisisitiza kwamba kwa pamoja, wanaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo, hivyo kuwanufaisha wakulima na kuimarisha uchumi wa taifa
No comments:
Post a Comment