Wahandisi Vijana nchini wameshauriwa kutumia fursa mbalimbali kupitia ujuzi na ubunifu waliokuwa nao ili kuwa wajasiriamali na kuleta mabadiliko chanya kwao na Taifa kwa ujumla.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhandisi, Zena Said leo, Septemba 4, 2024 wakati akifunga Jukwaa la Wahandisi Vijana jijini Dar es Salaam lililobebwa na kauli mbiu isemayo “Ujasiriamali na Uhandisi, kuongeza Kasi kwa Wahandisi Vijana kufikia Ubora” ambalo limeratibiwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).
“Nguvu ya Taifa letu ipo kwa vijana wake, mnategemewa kueta mabadiliko katika Sekta mbalimbali ndani ya nchi, Hivyo Wahandisi hasa vijana tumieni fursa hii ya ujasiriamali kujiajiri ili kujenga maisha bora kwenu na Taifa kwa ujumla”, amesema Katibu Mkuu Kiongozi.
Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa, Dkt.Samia Suluhu Hassan na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mheshimiwa, Dkt. Hussein Ally Mwinyi kwa kuendelea kutoa fursa kwa Wahandisi wa ndani kutekeleza miradi mbalimbali nchini.
Amewapongeza ERB kwa jitihada za kuhamasisha wanafunzi wa Kike kupenda masomo ya Sayansi hususan tasnia ya Uhandisi ambayo imekuwa ikitawaliwa na wanaume kwa muda mrefu.
Kadhalika, Mhandisi Said amewahimiza Wahandisi wote kuzingatia mabadiliko ya Teknolojia na kuendelea kutafuta fursa za kujifunza ili baadae kuja kusaidia kulijenga Taifa la Tanzania.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde amesema kuwa Jukwaa hilo limetoa ujuzi na maarifa ya kuunganisha dhana ya uhandisi na ujasiriamali ili kumwezesha Mhandisi kujiajiri na kukidhi mahitaji yake pamoja na kujenga uchumi wa nchi.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi, Mwanasheria Menye Manga amesema kuwa Jukwaa hilo ambalo limefanyika siku mbili limesaidia kubadilishana maarifa na mawazo ambayo yatakuwa chachu ya kuleta maendeleo nchini.
Ameongeza kuwa jumla ya Wahandisi 24 wamekula kiapo katika Kongamano hilo, na Wanafunzi 15 kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini waliofanya vizuri katika masomo ya uhandisi wamepewa vyeti.
Kongamano hili la siku mbili limehudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo wahandisi mbalimbali kutoka ndani ya nchi na nchi jirani za Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini, wadau mbalimbali pamoja na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao ya kihandisi kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment