Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ni nguzo muhimu katika afua za afya, Ustawi wa Jamii na Lishe.
Dkt. Kapologwe amebainisha hayo leo Septemba 4, 2024 katika Kikao Kazi cha Kuandaa Mpango wa Kuharakisha Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii nchini ambacho kimekutanisha Wadau wa sekta ya Afya kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa kushirikiana na Shirika la Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa la Afrika (Africa CDC) pamoja na Wadau wengine .
“Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wanatusaidia sana ikiwemo kupita kaya kwa kaya kutoa elimu ya afya na kudhibiti magonjwa hayo”amesema Dkt. Kapologwe.
Aidha, Dkt. Kapologwe amesema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wamekuwa mstari wa mbele katika utoaji wa taarifa kuhusu magonjwa ya mlipuko ambapo amesema ni askari na nguzo muhimu katika mapambano ya magonjwa kwenye jamii.
“Hawa ndio askari muhimu katika suala la kudhibiti magonjwa na kuimarisha afua za afya kwa matokeo chanya kwa jamii yetu”amesema.
Halikadhalika, Dkt. Kapologwe amezungumzia umuhimu wa ushirikiano katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii.
Lengo la Kikao hicho ni kujadili masuala ya Uratibu kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii na kupendekeza utaratibu ambapo wadau wanaotekeleza afua zinazohusiana na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wataweka Mipango ya Utekelezaji.
Ikumbukwe kuwa, Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ulizinduliwa tarehe 31, Januari, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango.
Kikao kazi hiki cha Kuandaa Mpango wa kuharakisha Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kinahusisha Watalaamu kutoka Wizara ya Afya (Bara na Visiwani), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Africa CDC, UNICEF, USAID, IRISH AID, Wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika (AU) na Wadau mbalimbali ambapo kimeanza Septemba 3, 2024 hadi Septemba 6, 2024 Jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment