Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya amesema Serikali kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) inaendelea kutekeleza miradi Saba ya ujenzi na ukarabati wa nyumba na majengo ya Serikali kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo fedha za ruzuku kutoka Serikalini.
Akizungumza wakati akiwasilisha taarifa kuhusu ujenzi na ukarabati wa nyumba na majengo ya Serikali unaosimamiwa na Wakala huo kwa kipindi cha Julai, 2023 hadi Septemba, 2024 Naibu Waziri Kasekenya amesema kuwa katika kipindi hicho Wakala ulipanga kutekeleza miradi Nane ambapo mradi mmoja kati ya hiyo umekamilika.
“Katika kipindi hiki cha Julai, 2023 hadi Septemba, 2024 TBA imetekeleza na inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa ghorofa za watumishi wa Umma za Kaloleni Kota jijini Arusha na Ghana Kota jijini Mwanza pamoja na ujenzi wa nyumba nyingine 20 za Viongozi jijini Dodoma”, amesema Kasekenya.
Aidha, Kasekenya ameongeza kuwa miradi hiyo ya ujenzi iliyotekelezwa inahusisha nyumba 356 ambapo nyumba 16 zilizopo Magomeni Kota zimekamilika na ujenzi wa nyumba 340 unaendelea huku jumla ya nyumba 20 zikikarabatiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mheshimiwa Selemani Kakoso ameitaka Wizara ya Ujenzi kuendelea kuisaidia TBA kukusanya madeni kwa Taasisi za Serikali, Wizara na watumishi wanaodaiwa Fedha za Pango na Wakala huo ili fedha zinazopatikana ziwezeshe Wakala kutekeleza miradi mingi zaidi.
Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Arch. Daud Kondoro amesema kuwa Wakala utaendelea na zoezi la ukusanyaji wa kodi kwa wapangaji wake na itachukua hatua kwa wadaiwa Sugu kama ambavyo imekwishaanza kufanya kwa baadhi ya mikoa ikiwemo Dar es Salaam.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi.
No comments:
Post a Comment