
Na Shua Ndereka
Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro Bi. Pilly Mwakasege amewakumbusha wananchi, kuendeleza mapambano ya kupinga ya rushwa kipindi cha uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2025.
“Wote tunajua shughuli iliyo mbele yetu juu ya uchaguzi wa serikali za mtaa na mwakani uchaguzi mkuu, hivyo tumetumia fursa hii kuongea na wanahabari,” alisema Mwakasege katika semina fupi kwa waandishi wa habari iliyofanyika katika ofisi za TAKUKURU zilizopo Manispaa ya Morogoro kwa lengo la uelimishaji wa masuala ya rushwa katika uchaguzi.
Ameongeza: “Sijawahi kuangushwa na wanahabari kote katika mikoa yote niliyopita kufanya kazi, wametupa ushirikiano na wametusaidia kuyafikia maeneo pengi hata tungeshindwa kufikia.”
Kabla ya kuhamishiwa mkoani Morogoro, Kamanda Mwakasege alikuwa Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kagera na ametumia fursa hiyo kujitambulisha kwa waandishi wa habari na kuomba ushirikiano, kwani anaamini wanahabari ni mabalozi wakubwa katika mapambano dhidi rushwa.
Kwa upande waeke Mkuu wa Dawati la Elimu kwa Umma TAKUKURU Mkoa wa Morogoro Bigambo Thomas amesema kuwepo kwa vitendo vya rushwa wakati wa uchaguzi, huwanyima HAKI wagombea na kuwakosesha maendeleo wananchi.
Akiwasilisha Mada katika semina kwa waandishi wa habari kuhusu ‘Rushwa kwenye uchaguzi’, Bigambo amebainisha kuwa, Vitendo vya rushwa kipindi cha uchaguzi vinazoofisha demokrasia, uhuru na haki ya kuchagua viongozi wanaofaa kwani mpiga kura anaweza kutumia dhamana yake kwa kujipatia manufaa binafsi badala ya kutekeleza jukumu lake la kuchagua viongozi bora wanaoweza kuleta maendeleo katika taifa.
“Upande wa wagombea wanaweza kutumia nafasi hiyo kugeuza uongozi kuwa bidhaa au kitu cha kununuliwa na hivyo kutumia pesa zao vibaya kwa lengo la kuwashawishi wapiga kura ili wawape nafasi za uongozi kwa manufaa yao binafsi,”amesema Bigambo.
Akieleza athari za rushwa katika uchaguzi, Bigambo amesema ni kupata kiongozi asiye na sifa zinazohitajika na jamii husika, rushwa inadhalilisha utu wa mtu kwa kulinganisha thamani ya kura yake na kitu au zawadi aliyopewa.
Bigambo amevikumbusha vyombo vya habari wajibu wao katika kuzuia Rushwa katika uchaguzi kuwa ni kuwaelimisha wananchi kuhusu rushwa, viashiria vya rushwa na madhara yake katika uchaguzi, kukataa kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa madhumuni ya kushawishika kumpigia kura mgombea aliyetoa zawadi, fedha au kitu chochote cha thamani.
Pia kushiriki kwenye mikutano ya kampeni ili kujua sera za wagombea na vyama vyao ili ziwawezeshe kuchagua kiongozi atakayewajibika kwenye jamii na kukuza uandishi wa habari za kiuchunguzi ili kuibua vitendo vya rushwa na udanganyifu kwenye uchaguzi na Kutoa taarifa za viashiria na vitendo vya rushwa.
Akitoa shukrani kwa niaba ya waandishi wa habari, Mratibu wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Morogoro (MORO PRESS CLUB) Thadei Hafigwa ameishukuru TAKUKURU kwa mwaliko wao kwa waandishi wa habari huku akiomba mafunzo hayo kuwa endelevu hasa katika masuala ya sheria.

No comments:
Post a Comment