Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Jerry Silaa, amezindua mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa katika kijiji cha Hika Kata ya Makuru, wilayani Manyoni Mkoani Singida.
Mnara huo uliojengwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mwasiliano kwa Wote (UCSAF), ni muendelezo wa juhudi za Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini ili kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo hayo.
Waziri Silaa ameongeza kwa kusema kuwa, dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa maeneo ya vijijini yanafikiwa na huduma bora za mawasiliano ikiwemo mtandao wa intaneti;
"Dhamira yetu ya kimkakati ya kuimarisha muunganisho katika maeneo ya vijijini, na sasa tunafanya uboreshaji mkubwa wa minara ya mawasiliano inayofanya kazi kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G/4G," alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, ameishukuru Serikali na kuongeza kuwa, sasa wananchi wa Kata ya Makuru na vijiji vyake wanaweza kutumia mawasiliano ya simu kuboresha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Gharama ya jumla ya ujenzi wa manara huo ni shilingi milioni 272 kati ya hizo UCSAF imetoa ruzuku ya shilingi milioni 118 na TTCL imetoa zaidi ya shilingi milioni 150. Jumla ya wananchi takribani 24,000 katika kijiji cha Hila, Londoni na Msemembo na vijiji vya jirani watanufaika na kuwepo kwa mnara huo.
Waziri Silaa yuko Mkoani Singida kwa ziara ya siku tano yenye lengo la kukagua, kutembelea na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo, kauli mbiu ikiwa ni; “RAIS SAMIA NA MAENDELEO, WASIKIE NA WAONE”.
No comments:
Post a Comment