Wanafunzi wapya wakaribishwa TEWW, wahimizwa kuzingatia malengo yaliyowaleta - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, November 1, 2024

Wanafunzi wapya wakaribishwa TEWW, wahimizwa kuzingatia malengo yaliyowaleta

Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Philipo Sanga akiongea na wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa taasisi hiyo wakati wa kuhitimisho la mafunzo ya awali (Orientation Course) leo Novemba 1, 2024 makao makuu ya TEWW mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya wanafunzi wapya wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) kwa mwaka wa masomo 2024/2025 wakimsikiliza Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu WazimTEWW, Prof. Philipo Sanga (hayupo pichani) wakati wa hitimisho la mafunzo ya awali (Orientation Course) leo Novemba 1, 2024 makao makuu ya TEWW mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.

Wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Taasisi ya Elimu ya Watu wa Wazima (TEWW) kwa mwaka wa masomo 2024/2025 wamekaribishwa rasmi huku wakihimizwa kuzingatia malengo yaliyowaleta masomoni ili waweze kuhitimu vyema.

Pia, wanafunzi hao wameshauriwa kutokata tamaa pindi wapatapo changamoto, bali wawe wastahimilivu na waziwasilishe kwenye mamlaka ili zipatiwe ufumbuzi.

Hayo yamesemwa leo Novemba 1, 2024 na Kaimu Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, Prof. Philipo Sanga wakati wa kuhitimisha Mafunzo ya Awali (Orientation Course) kwa wanafunzi hao yaliyofanyika Makao Makuu ya TEWW, mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.

Prof. Sanga amesema kuwa kila mwanafunzi aliyeripoti masomoni amefanya hivyo akiwa na malengo maalum yatakayomsukuma kumaliza masomo licha ya changamoto zitakazojitokeza.

“Mmekuja kuanza masomo...hii ni safari mmeianza, hivyo ni muhimu sana kutarajia mwisho tangu mwanzo...kwamba mmekuja kusoma ili siku moja mhitimu kwa sababu katika hatua hii ya utu uzima tunajua wote hapa mmekuja mkiwa na malengo,” amesema Prof. Sanga.

Ameongezea kuwa taasisi yake imeijipanga kuwahudumia kwa kuzingatia malengo yao na kuwasaidia kutatua changamoto watakazokutana nazo ili waweze kumaliza masomo yao.

“Sisi pia tunatamani tuwahudumie kwa kuzingatia mna malengo yenu na mpatapo changamoto sisi sote kwa ujumla wetu tutajitahidi sana kuwasaidia ili changamoto ziishe na hatimaye muweze kufikia malengo yenu,” amesema.

Aidha, kiongozi huyo amewasisitiza wanafunzi hao wapatapo changamoto yoyote wasione ndiyo mwisho, bali watambue yapo majawabu yatakayowasaidia kuhitimu masomo yao.

TEWW ni taasisi ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliyoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 12 ya mwaka 1975. Pamoja na mambo mengine taasisi hii inajukumu la kutoa elimu ya kujiendeleza na mafunzo ya elimu ya watu wazima kupitia njia ya elimu masafa (distance learning) na ana kwa ana.

Taasisi hii yenye vituo mikoa yote 26 ya Tanzania Bara inatoa elimu ya ngazi ya Astashahada, Stashahada, na Shahada. Pia, inatoa elimu ya sekondari kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi. Vilevile, inatoa elimu ya ujasiriamali, stadi za maisha na ufundi.

Desemba 12 mwaka huu TEWW inatarajia kufanya mahafali yake ya 63 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975, ambapo wahitimu takriban 488 wanatarajiwa kutunikiwa vyeti katika ngazi mbalimbali.

No comments:

Post a Comment