WATAALAMU WA HOSPITALI YA KANDA MBEYA WAWASILI CHUNYA KWENYE KAMBI YA MATIBABU YA MTOTO WA JICHO, ZAIDI YA WAGONJWA 500 KUNUFAIKA KAMBI HIYO. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, November 18, 2024

WATAALAMU WA HOSPITALI YA KANDA MBEYA WAWASILI CHUNYA KWENYE KAMBI YA MATIBABU YA MTOTO WA JICHO, ZAIDI YA WAGONJWA 500 KUNUFAIKA KAMBI HIYO.


Wataalamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya leo wamewasili wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya kutoa huduma mkoba ya matibabu ya kibingwa ya mtoto wa jicho kwa siku 7, ambapo zaidi ya wagonjwa 500 wanatarajiwa kunufaika na kambi hiyo inayoratibiwa na Shirika la Helen Keller International (HKI) kwa kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, na kufanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya, ikiwa ni juhudi za kupunguza tatizo la upofu nchini Tanzania inatarajiwa kufanyika kwa siku saba

Akiongea na washiriki wa kambi hiyo Daktari Bingwa wa macho na Kiongozi wa timu ya wataalamu hao Dkt. Barnabas Mshangila ameeleza kuwa kambi hiyo inatoa fursa kwa wagonjwa wengi ambao hawana uwezo wa kugharamia matibabu ya Mtoto wa jicho na kuwasaidia kuondokana na matatizo hayo na kuboresha maisha yao kupitia upasuaji wa mtoto wa jicho.
“Timu imejipanga vizuri katika kutoa huduma za matibabu ya kibingwa. Tumejipanga kwa kila hali na tunatarajia kutoa huduma bora kwa wagonjwa wetu. Ni muhimu kuhakikisha kwamba kila mtu anayehitaji huduma za macho anapata matibabu stahiki.”- Dkt. Mshangila

Nae Dkt. Fariji Kilewa Mratibu wa huduma za macho mkoa wa Mbeya pia aliongeza, “Huduma kama hizi ni muhimu sana katika jamii zetu, na tunawashukuru wadau wote wanaohusika katika kutekeleza mradi huu. Ushirikiano wa pamoja unasaidia kufanikisha malengo yetu ya kutoa matibabu bora kwa wagonjwa wa Mtoto wa jicho.”

Kwa upande wake, Allen Lemilia Afisa Mradi kutoka Shirika lisilo la Kiserikali la Helen Keller, alisema kuwa shirika hilo litaendelea kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za matibabu ya macho kwa wananchi walio maeneo mbali na maeneo ya kutolea huduma za afya kwa kufanya huduma mkoba katika kupeleka wataalamu pamoja na vifaa tiba vya kutolea huduma ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo na kupunguza gharama kwa jamii kuungana pamoja kutimiza malengo ya kupunguza tatizo la upofu katika mkoa wa Mbeya, na kwa pamoja kuweza kubadili maisha ya watu wengi kwa kutoa huduma bora za afya.

“Tunatambua changamoto za watu ambao hawana uwezo wa kupata matibabu haya ya mtoto wa jicho. Kambi hii ni muhimu katika kuhakikisha kwamba jamii wanaweza kupata matibabu ya macho na kuondokana na matatizo yanayoweza kuathiri maono yao na maisha yao ya baadaye. Kwa hiyo, tutaendelea kutoa huduma hizi katika kuiunga mkono Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha huduma za matibabu ya macho,” aliongeza Allen.





No comments:

Post a Comment